Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 9:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yesu aliwaita wale kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuponya pepo wote, na uwezo wa kuponya wagonjwa.

2. Halafu akawatuma waende kuhubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

3. Akawaambia, “Mnaposafiri msichukue chochote: Msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada.

4. Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho.

5. Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo, nanyi mnapotoka kunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.”

6. Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

7. Sasa, mtawala Herode alipata habari za mambo yote yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema: “Yohane amefufuka kutoka kwa wafu!”

8. Wengine walisema kwamba Elia ametokea, na wengine walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani.

9. Lakini Herode akasema, “Huyo Yohane nilimkata kichwa; sasa ni nani huyu ninayesikia habari zake?” Akawa na hamu ya kumwona.

10. Wale mitume waliporudi, walimweleza Yesu yote waliyoyafanya. Yesu akawachukua, wakaenda peke yao mjini Bethsaida.

11. Lakini wale watu walipojua alikokwenda, walimfuata. Yesu akawakaribisha akawazungumzia juu ya ufalme wa Mungu, akawaponya wale waliohitaji kuponywa.

12. Jua lilipokuwa linaanza kutua, wale kumi na wawili walimwendea wakamwambia, “Waage watu waende kwenye vijiji na mashamba ya karibu, wakajipatie chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tulipo ni nyikani.”

13. Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Wakamjibu, “Hatuna chochote ila mikate mitano na samaki wawili. Labda twende wenyewe tukawanunulie chakula watu wote hawa!”

14. (Walikuwapo pale wanaume wapatao 5,000.) Basi, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waambieni watu waketi katika makundi ya watu hamsinihamsini.”

Kusoma sura kamili Luka 9