Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 14:2-15 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Mbele yake Yesu palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kuvimba mwili.

3. Yesu akawauliza waalimu wa sheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?”

4. Lakini wao wakakaa kimya. Yesu akamshika huyo mgonjwa, akamponya, akamwacha aende zake.

5. Halafu akawaambia, “Ni nani kati yenu ambaye mtoto wake au ng'ombe wake akitumbukia shimoni, hangemtoa hata kama ni siku ya Sabato?”

6. Nao hawakuweza kumjibu swali hilo.

7. Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano:

8. “Kama mtu akikualika harusini, usiketi mahali pa heshima, isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe;

9. na mwenyeji wenu nyinyi wawili atakuja na kukuambia: ‘Mwachie huyu nafasi.’ Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho.

10. Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akuambie: ‘Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi.’ Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe.

11. Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa na anayejishusha, atakwezwa.”

12. Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, “Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri wasije nao wakakualika, nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea.

13. Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema, viwete na vipofu,

14. nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka.”

15. Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, “Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika ufalme wa Mungu.”

Kusoma sura kamili Luka 14