Agano la Kale

Agano Jipya

1 Yohane 2:4-22 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake.

5. Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye:

6. Mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.

7. Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia.

8. Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa kweli umekwisha anza kuangaza.

9. Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani.

10. Yeyote ampendaye ndugu yake yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine.

11. Lakini anayemchukia ndugu yake yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha.

12. Ninawaandikieni nyinyi watoto kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo.

13. Nawaandikieni nyinyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo.Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu.

14. Nawaandikieni nyinyi watoto kwa sababu mnamjua Baba.Nawaandikieni nyinyi kina baba kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo.Nawaandikieni nyinyi vijana kwa sababu mna nguvu;neno la Mungu limo ndani yenuna mumemshinda yule Mwovu.

15. Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake.

16. Vitu vyote vya ulimwengu – tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali – vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu.

17. Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele.

18. Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba mpinzani wa Kristo anakuja, na sasa wapinzani wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu.

19. Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu.

20. Nyinyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli.

21. Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamwujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli.

22. Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Kristo. Mtu wa namna hiyo ni mpinzani wa Kristo – anamkana Baba na Mwana.

Kusoma sura kamili 1 Yohane 2