Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 7:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile.

8. Basi, wale ambao hawajaoa na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo.

9. Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia, basi na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa.

10. Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: Mke asiachane na mumewe;

11. lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe.

12. Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka.

13. Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe.

14. Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu.

15. Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni nyinyi muishi kwa amani.

16. Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo?

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 7