Agano la Kale

Agano Jipya

Neh. 9:1-18 Swahili Union Version (SUV)

1. Hata siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Israeli wakawa wamekusanyika, wakifunga, wenye kuvaa magunia, na kujitia udongo vichwani.

2. Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao.

3. Basi wakasimama mahali pao, wakasoma katika kitabu cha torati ya BWANA, Mungu wao, muda wa robo ya siku; na robo nyingine wakaungama, wakamwabudu BWANA, Mungu wao.

4. Ndipo wakasimama madarajani pa Walawi, Yeshua, na Bani, na Kadmieli, na Shebania, na Buni, na Sherebia, na Bani, na Kenani, wakamlilia BWANA, Mungu wao, kwa sauti kuu.

5. Ndipo Walawi, Yeshua na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethahia, wakasema, Simameni, mkamhimidi BWANA, Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.

6. Ezra akasema, Wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako; wewe ulifanya mbingu, mbingu za mbingu, pamoja na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vitu vyote vilivyomo, nawe unavihifadhi vitu hivi vyote; na jeshi la mbinguni lakusujudu wewe.

7. Wewe ndiwe BWANA, Mungu, uliyemchagua Abramu, na kumtoa katika Uri wa Wakaldayo, na kumpa jina la Ibrahimu;

8. nawe ukauona moyo wake kuwa mwaminifu mbele zako, ukafanya agano naye, kumpa nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Myebusi, na Mgirgashi, naam, kuwapa wazao wake; nawe umeyafikiliza maneno yako, kwa kuwa ndiwe mwenye haki.

9. Tena uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya bahari ya Shamu;

10. nawe ukaonyesha ishara nyingi na mambo ya ajabu juu ya Farao, na juu ya watumishi wake wote, na juu ya watu wote wa nchi yake; kwa maana ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina kama vile ilivyo leo.

11. Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, mfano wa jiwe katika maji makuu.

12. Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.

13. Tena ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;

14. ukawajulisha sabato yako takatifu, na kuwaagiza maagizo, na amri, na sheria, kwa mkono wa mtumishi wako, Musa.

15. Ukawapa chakula toka mbinguni, kwa ajili ya njaa yao, na kwa ajili yao ukaleta maji kutoka mwambani, kwa sababu ya kiu yao, ukawaamuru kwamba waingie katika nchi na kuimiliki, ambayo umeinua mkono wako kuwapa.

16. Lakini wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wala hawakuzisikiliza amri zako,

17. ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.

18. Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;

Kusoma sura kamili Neh. 9