Agano la Kale

Agano Jipya

Neh. 6:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);

2. Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya.

3. Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?

4. Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.

5. Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;

6. nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.

7. Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja.

8. Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.

9. Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.

10. Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, tukaifunge milango ya hekalu; kwa maana watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.

Kusoma sura kamili Neh. 6