Agano la Kale

Agano Jipya

Mdo 26:10-28 Swahili Union Version (SUV)

10. nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nalitoa idhini yangu.

11. Na mara nyingi katika masinagogi yote naliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini.

12. Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani;

13. Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.

14. Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.

15. Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.

16. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;

17. nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;

18. uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

19. Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni,

20. bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.

21. Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata ndani ya hekalu wakajaribu kuniua.

22. Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa;

23. ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.

24. Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili.

25. Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.

26. Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.

27. Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.

28. Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo.

Kusoma sura kamili Mdo 26