Agano la Kale

Agano Jipya

Ebr. 11:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.

2. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa.

3. Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.

4. Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena.

5. Kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.

6. Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.

7. Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

8. Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.

9. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

11. Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.

12. Na kwa ajili ya hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na kama mchanga ulio ufuoni, usioweza kuhesabika.

13. Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi.

14. Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.

15. Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.

16. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.

Kusoma sura kamili Ebr. 11