Agano la Kale

Agano Jipya

Zekaria 14:3-16 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Kisha Mwenyezi-Mungu atatoka na kuyapiga vita mataifa hayo, kama afanyavyo daima siku za vita.

4. Siku hiyo, atasimama kwenye mlima wa mizeituni ulio mashariki ya mji wa Yerusalemu. Mlima huo utagawanywa sehemu mbili na bonde pana sana litatokea toka mashariki hadi magharibi. Nusu moja itaelekea kaskazini na nusu nyingine kusini.

5. Nyinyi mtakimbia kupitia bonde hilo, katikati ya milima miwili ya Mwenyezi-Mungu. Mtakimbia kama wazee wenu walivyokimbia tetemeko la ardhi wakati wa utawala wa mfalme Uzia wa Yuda. Kisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye.

6. Wakati huo hakutakuwa baridi wala baridi kali.

7. Mchana utaendelea bila giza kuingia. Wakati huo wajulikana kwa Mwenyezi-Mungu peke yake. Hakutakuwa mchana wala usiku, kwa maana hata saa za jioni mwanga utaendelea kuwapo.

8. Wakati huo, maji ya uhai yatabubujika kutoka mji wa Yerusalemu, na nusu ya maji hayo yatatiririkia kwenye bahari ya mashariki, na nusu nyingine kwenye bahari ya magharibi. Maji hayo yataendelea kububujika wakati wa kiangazi kama yalivyo wakati wa masika.

9. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye mfalme pekee wa dunia yote; naye atakuwa ndiye Mwenyezi-Mungu pekee, mmoja tu, na jina lake litakuwa ndilo jina pekee.

10. Nchi yote, tangu Geba hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itageuzwa kuwa mbuga tambarare kabisa. Lakini mji wa Yerusalemu utabaki juu mahali pake tokea lango la Benyamini mpaka lango la zamani, hadi kwenye lango la Konani, tangu mnara wa Hanareli hadi kwenye mashinikizo ya mfalme.

11. Mji wa Yerusalemu utakaliwa na watu kwani ndani yake haitakuwapo laana tena; naam, watu watakaa humo kwa usalama.

12. Lakini kuhusu wale watu ambao walikuja kupigana na Yerusalemu, haya ndiyo maafa ambayo Mwenyezi-Mungu atawaletea: Miili yao itaoza wangali hai; macho yao yataoza yakiwa kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza zikiwa vinywani mwao.

13. Siku hiyo, hofu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu itawakumba watu, na kila mtu atamshambulia mwenzake.

14. Watu wa Yuda watapigana kuulinda mji wa Yerusalemu; utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka nchi ya Yuda utakusanywa: Watakusanya dhahabu, fedha na mavazi kwa wingi sana.

15. Maafa makubwa yatawakumba farasi, nyumbu, ngamia, punda na wanyama wote watakaokuwamo katika kambi hizo za maadui.

16. Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda.

Kusoma sura kamili Zekaria 14