Agano la Kale

Agano Jipya

Zaburi 38:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;usiniadhibu kwa ghadhabu yako.

2. Mishale yako imenichoma;mkono wako umenigandamiza.

3. Hamna mahali nafuu mwilini mwangu,kwa sababu umenikasirikia;hamna penye afya hata mifupani mwangu,kwa sababu ya dhambi yangu.

4. Nimefunikwa kabisa na dhambi zangu,zinanilemea kama mzigo mzito mno kwangu.

5. Madonda yangu yameoza na kunuka,na hayo ni matokeo ya ujinga wangu.

6. Nimepindika mpaka chini na kupondeka;mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.

7. Viungo vyangu vimeshambuliwa na homa;mwilini mwangu hamna nafuu yoyote.

8. Nimelegea na kupondekapondeka;nasononeka kwa kusongwa moyoni.

9. Ee Bwana, wewe wajua tazamio langu lote;kwako hakikufichika kilio changu.

10. Moyo wanidunda, nguvu zimeniishia;hata macho yangu nayo yamekwisha fifia.

11. Rafiki na wenzangu wanaepa kuona mateso yangu,na jamaa zangu wanakaa mbali nami.

12. Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao;wanaonitakia niumie wanatishia kuniangamiza.Mchana kutwa wanafanya mipango dhidi yangu.

13. Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii;nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu.

Kusoma sura kamili Zaburi 38