Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 8:22-34 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Watu waliobaki mjini walitoka, lakini wote wakawa wamezingirwa na Waisraeli; nao wakauawa, asibaki hata mmoja wao.

23. Lakini mfalme wa mji wa Ai walimteka akiwa hai na kumpeleka kwa Yoshua.

24. Waisraeli walipomaliza kabisa kuwaua watu wote wa Ai huko nyikani ambako waliwafuatia wakarudi mjini Ai na kuwaua wote waliosalia humo.

25. Jumla ya watu wa Ai waliouawa siku hiyo, wanaume kwa wanawake, walikuwa 12,000.

26. Yoshua hakuushusha mkono wake aliokuwa ameushikilia mkuki wake kuelekea Ai mpaka alipowaua wakazi wote wa mji huo.

27. Waisraeli waliteka tu wanyama na mali kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua.

28. Basi, Yoshua aliuteketeza mji wa Ai kwa moto na kuufanya magofu hadi hivi leo.

29. Kisha akamtundika mfalme wa Ai mtini mpaka jioni. Lakini jua lilipoanza kutua, Yoshua aliamuru maiti yake iondolewe mtini na kutupwa kwenye lango la mji kisha warundike rundo kubwa la mawe juu ya maiti hiyo; rundo hilo liko huko mpaka leo.

30. Kisha, Yoshua akamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, madhabahu mlimani Ebali,

31. kama Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Waisraeli, kadiri ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria ya Mose kwamba itakuwa madhabahu iliyojengwa kwa mawe ambayo hayakuchongwa, wala kuguswa na chombo chochote cha chuma. Juu ya madhabahu hiyo walimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za kuteketezwa na sadaka za amani.

32. Na huko, mbele ya umati wote wa Waisraeli, Yoshua aliandika nakala ya sheria ya Mose juu ya mawe.

33. Waisraeli wote pamoja na viongozi wao, wazee na waamuzi na wageni wote waliokuwa kati yao, wakasimama kila upande mkabala na sanduku la agano mbele ya makuhani Walawi waliokuwa wamelibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Nusu yao wakasimama mbele ya mlima Gerizimu na nusu nyingine wakasimama mbele ya mlima Ebali, kama vile Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyoagiza hapo awali kuhusu kubarikiwa kwa Waisraeli.

34. Kisha, Yoshua akawasomea sheria zote, pamoja na baraka na laana kama ilivyoandikwa katika kitabu cha sheria.

Kusoma sura kamili Yoshua 8