Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 24:23-33 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Naye akawaambia, “Basi, ondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mkamfuate Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wenu wote.”

24. Nao, wakasema, “Tutamtumikia na kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.”

25. Hivyo, Yoshua akafanya agano na Waisraeli huko Shekemu, akawapa masharti na maagizo ya kufuata.

26. Yoshua akayaandika haya yote katika kitabu cha sheria ya Mungu; kisha, akachukua jiwe kubwa na kulisimika chini ya mwaloni katika hema ya Mwenyezi-Mungu.

27. Halafu akawaambia watu wote, “Jiwe hili ndilo litakalokuwa shahidi kwetu, maana limesikia maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu ametuambia. Kwa hiyo, litashuhudia dhidi yenu, ili msije mkamkana Mungu wenu.”

28. Halafu Yoshua akawaruhusu watu waondoke; nao wakaenda kila mmoja kwake.

29. Baada ya mambo hayo, Yoshua, mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, akafariki akiwa na umri wa miaka 110.

30. Nao wakamzika kwenye eneo ambalo alikuwa amegawiwa kuwa sehemu yake, huko Timnath-sera, katika milima ya Efraimu, kaskazini ya mlima wa Gaashi.

31. Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu muda wote wa uhai wa Yoshua, na baada ya kifo chake, waliendelea kumtumikia kwa muda walioishi wale wazee waliokuwa wameona kwa macho yao mambo yale Mwenyezi-Mungu aliyowatendea Waisraeli.

32. Mifupa ya Yosefu ambayo Waisraeli walikuwa wameileta kutoka Misri waliizika huko Shekemu katika eneo ambalo Yakobo alikuwa amelinunua kutoka kwa wana wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha. Ardhi hii nayo ikawa mali yao wazawa wa Yosefu.

33. Naye Eleazari, mwana wa Aroni, akafariki na kuzikwa Gibea, mji ambao alikuwa amepewa mwanawe Finehasi katika nchi ya milima ya Efraimu.

Kusoma sura kamili Yoshua 24