Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 23:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Mtu wenu mmoja tu anaweza kuwakimbiza maadui elfu, kwani Mwenyezi-Mungu Mungu wenu ndiye anayewapigania kama alivyowaahidi.

11. Basi, muwe waangalifu sana kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

12. Maana, kama mkimwasi Mwenyezi-Mungu na kujiunga na mataifa haya yaliyobaki kati yenu, mkaoa kwao nao wakaoa kwenu,

13. jueni kwa hakika kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hataendelea kuyafukuza mataifa haya mbele yenu, bali yatakuwa kwenu kikwazo na mtego. Yatakuwa kwenu mjeledi wa kuwachapeni na miiba ya kuwachomeni machoni mpaka hapo mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni.

14. “Sasa, wakati wangu wa kufariki dunia kama ilivyo kawaida ya walimwengu wote umekaribia. Lakini nyinyi nyote mnajua wazi mioyoni na rohoni mwenu kwamba katika mambo yote mema ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wenu aliwaahidi, hakuna hata moja ambalo halikutimia. Yote yametimia kama vile alivyoahidi.

15. Lakini kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyotimiza mambo yote mema aliyowaahidi, vivyo hivyo anaweza kuwaletea maovu yote mpaka awaangamize nyote kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni.

16. Kama mkivunja agano lake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru mlishike, mkaenda kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, nanyi mtaangamia mara moja kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni.”

Kusoma sura kamili Yoshua 23