Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 22:27-34 Biblia Habari Njema (BHN)

27. bali tulitaka madhabahu hii iwe ushuhuda kati yetu na nyinyi na vizazi vyetu vijavyo kwamba sisi tunayo haki ya kumtumikia Mwenyezi-Mungu kwa sadaka zetu za kuteketezwa na tambiko zetu, na kwa sadaka zetu za amani, ili watoto wenu wasije wakawaambia watoto wetu kwamba hawana fungu lolote lao kwa Mwenyezi-Mungu.

28. Tena tulifikiri kwamba ikiwa jambo kama hilo litasemwa juu yetu au juu ya wazawa wetu katika siku zijazo, tutasema, ‘Tazameni mfano wa madhabahu ya Mwenyezi-Mungu ambayo wazee wetu waliijenga; sio kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka au tambiko bali kama ushuhuda kati yetu na nyinyi’.

29. Sisi hatukuwa na nia ya kumwasi sasa Mwenyezi-Mungu hata kidogo na kumwacha kwa kujenga madhabahu ya kutolea sadaka za kuteketezwa au sadaka za unga au za tambiko. Hatupendi kutolea sadaka mahali pengine isipokuwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake.”

30. Kuhani Finehasi, viongozi wa jumuiya nzima na wakuu wa jamaa za Israeli waliokuwa pamoja naye waliposikia maneno hayo ya watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakaridhika.

31. Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akayaambia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, “Leo tumejua kwamba Mwenyezi-Mungu yumo miongoni mwenu maana hamkumfanyia Mungu uasi. Sasa mmewaokoa Waisraeli wasiadhibiwe na Mwenyezi-Mungu.”

32. Basi, Finehasi mwana wa kuhani Eleazari pamoja na viongozi wenzake wakawaaga watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaondoka nchini Gileadi, wakarudi Kanaani kwa Waisraeli na kuwapa habari hizo.

33. Taarifa hiyo ikawafurahisha Waisraeli, wakamshukuru Mwenyezi-Mungu na kuacha mipango yao ya vita na lengo lao la kuharibu kabisa nchi iliyokuwa ya makabila ya Reubeni na Gadi.

34. Watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaiita ile madhabahu ya “Ushuhuda,” kwani walisema, “Madhababu hii ni ushahidi wetu kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.”

Kusoma sura kamili Yoshua 22