Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 18:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya kuishinda ile nchi, jumuiya yote ya Waisraeli ilikusanyika huko Shilo na kulisimika hema la mkutano.

2. Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ambayo hayakuwa yamegawiwa sehemu yao ya nchi.

3. Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni?

4. Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa.

5. Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini.

6. Tayarisheni maelezo kamili juu ya sehemu zote saba na kuniletea. Hapo, nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kuhusu sehemu ya kila kabila lenu.

7. Lakini Walawi hawatapata sehemu yoyote kati yenu, maana sehemu yao ni kuwa makuhani wa kumhudumia Mwenyezi-Mungu. Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase walikwisha pata sehemu yao upande wa mashariki wa mto Yordani. Walipewa sehemu hii na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.”

8. Basi, watu hao wakaanza safari ya kwenda kuichunguza nchi. Kabla hawajaenda, Yoshua akawapa maagizo: “Nendeni nchini kote mkaandike maelezo kamili juu ya hiyo nchi, kisha mrudi mnieleze, nami nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu hapa hapa Shilo kuhusu sehemu mtakayopewa.”

9. Wanaume hao wakazunguka nchini kote, wakachora maelezo kamili juu ya sehemu zake saba pamoja na miji yake, kisha wakarudi kwa Yoshua kule kambini Shilo.

10. Huko Shilo, Yoshua akazipigia kura sehemu hizo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawagawia Waisraeli; kila kabila na sehemu yake.

11. Kura ya kwanza ililipata kabila la Benyamini kulingana na koo zake. Eneo walilopewa watu hao lilikuwa katikati ya lile la kabila la Yuda na lile la kabila la Yosefu.

Kusoma sura kamili Yoshua 18