Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 13:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati huu, Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe sasa umekuwa mzee wa miaka mingi, na kumebaki bado sehemu kubwa za nchi ambazo hazijatwaliwa.

2. Sehemu hizo ni: Nchi yote ya Wafilisti na nchi yote ya Wageshuri,

3. yaani eneo lijulikanalo kama la Wakanaani, kuanzia kijito cha Shihori mpakani mwa Misri hadi eneo la Ekroni huko kaskazini. Maeneo yote ya watawala watano wa Ufilisti: Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni pamoja na eneo la Avi,

4. upande wa kusini. Hali kadhalika nchi za Wakanaani kuanzia Ara ya Wasidoni mpaka Afeka mpakani mwa Waamori;

5. vilevile eneo la Gebali na Lebanoni mashariki ya Baal-gadi chini ya mlima Hermoni mpaka Lebo-hamathi;

6. pia eneo la milima iliyo kati ya Lebanoni na Misrefoth-maimu ambayo wakazi wake ni Wasidoni. Kadiri Waisraeli watakavyoendelea katika nchi hizo, mimi mwenyewe nitayafukuza mataifa hayo mbele yao. Nawe utawagawia Waisraeli sehemu mbalimbali za nchi hizo kwa kura kama nilivyokuamuru.

7. Utayagawia nchi hizo makabila tisa na nusu ya kabila la Manase ambayo bado hayajapata kitu.”

8. Makabila ya Reubeni, Gadi na nusu nyingine ya kabila la Manase yalikuwa yamepewa nchi iliyo mashariki ya mto Yordani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, mtumishi wake.

9. Eneo lao lilikuwa kuanzia Aroeri ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ule ulio katikati ya bonde, na nchi ile yote ya tambarare tangu Medeba mpaka Diboni,

10. pamoja na miji ya mfalme Sihoni wa Waamori, aliyetawala huko Heshboni hadi mpakani mwa Waamoni,

11. pamoja na nchi za Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaakathi, mlima wa Hermoni na nchi yote ya Bashani mpaka Saleka;

12. na ufalme wote wa Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala huko Ashtarothi na Edrei katika Bashani. Mose alikuwa amewashinda hao wote na kuwafukuzia mbali.

13. Hata hivyo, Wageshuri na Wamaaka hawakufukuzwa bali wanaishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo.

14. Mose hakuwapa watu wa kabila la Lawi nchi yoyote. Bali tambiko walizomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli kwa moto, hizo ndizo zilizokuwa fungu lao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose.

Kusoma sura kamili Yoshua 13