Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 11:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mfalme Yabini wa mji wa Hazori alipopata habari hizo, alipeleka ujumbe kwa mfalme Yobabu wa Madoni, mfalme wa Shimroni na mfalme wa Akshafi,

2. na kwa wafalme waliokuwa katika milima ya kaskazini, waliokuwa Araba ambayo ilikuwa kusini mwa Kinerethi, kwenye tambarare na waliokuwa Nafath-dori katika upande wa magharibi.

3. Pia, alipeleka ujumbe kwa Wakanaani waliokuwa pande za mashariki na magharibi, kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wayebusi ambao walikaa milimani na kwa Wahivi ambao walikaa chini ya mlima Hermoni katika nchi ya Mizpa.

4. Basi, wakatoka wote na majeshi yao makubwa. Nao walikuwa wengi kama mchanga wa pwani pamoja na magari mengi na farasi wengi sana.

5. Wafalme hawa wote wakaungana na kupiga kambi yao katika chemchemi ya Meromu ili wapigane na Waisraeli.

6. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hao, maana kesho, wakati kama huu, nitawaangamiza wote kwa kuwatia mikononi mwa Waisraeli; nanyi mtakata mishipa ya farasi wao na kuteketeza magari yao kwa moto.”

7. Basi, ghafla kwenye chemchemi ya Meromu Yoshua pamoja na jeshi lake lote akawatokea na kuwashambulia.

8. Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Waisraeli, nao wakawachapa na kuwafukuza mpaka Sidoni Kuu na Misrefoth-maimu, hadi upande wa mashariki katika bonde la Mizpa. Waisraeli wakawapiga na kuwaua wote.

9. Yoshua aliwakatakata mishipa farasi wao wote na kuyateketeza magari yao kwa moto, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza.

10. Yoshua alipokuwa anarudi, akauteka mji wa Hazori. Alimuua mfalme wake maana ndiye aliyekuwa kiongozi wa falme hizo zote.

Kusoma sura kamili Yoshua 11