Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 10:24-33 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Wafalme hao walipoletwa, Yoshua akawaita Waisraeli wote na wakuu wa majeshi waliokwenda naye vitani, akawaambia, “Njoni karibu mwakanyage wafalme hawa shingoni mwao.” Nao wakasogea na kuwakanyaga shingoni.

25. Yoshua akawaambia “Msiogope, wala msiwe na wasiwasi, muwe imara na hodari, maana hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyowatendea adui zenu ambao mtapigana nao. Kwa hiyo, muwe imara na hodari.”

26. Baadaye, Yoshua aliwanyonga kwa kuwaangika kwenye miti mitano ambako walitundikwa mpaka jioni.

27. Wakati jua lilipokuwa karibu kutua, Yoshua aliamuru waondolewe juu ya miti walipokuwa wameangikwa na kutupwa pangoni walimokuwa wamejificha. Kisha wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, nayo mawe hayo yako huko mpaka leo.

28. Siku hiyo Yoshua alipouteka mji wa Makeda, alimuua mfalme wake na wakazi wake wote bila kumbakiza hata mtu mmoja. Alimtendea mfalme wa Makeda kama vile alivyomtendea mfalme wa Yeriko.

29. Kutoka Makeda, Yoshua pamoja na Waisraeli wote walikwenda Libna wakaushambulia.

30. Mwenyezi-Mungu akautia mji huo pamoja na mfalme wao mikononi mwa Waisraeli, wakawaua wakazi wake bila kumbakiza hata mtu mmoja. Walimtendea mfalme wa Libna kama walivyomtendea mfalme wa Yeriko.

31. Kisha kutoka Libna Yoshua na Waisraeli wote walikwenda Lakishi, wakauzingira na kuushambulia.

32. Naye Mwenyezi-Mungu akautia mji huo mikononi mwa Waisraeli, wakauteka mnamo siku ya pili. Waliwaua wakazi wote wa mji huo kama walivyofanya kule Libna.

33. Hapo, mfalme Horamu wa Gerezi akaamua kuja kuwasaidia watu wa Lakishi. Lakini Yoshua alimuua pamoja na watu wake wote, hakumbakiza hata mtu mmoja.

Kusoma sura kamili Yoshua 10