Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 7:5-17 Biblia Habari Njema (BHN)

5. “Ila kama mkibadili mienendo yenu na matendo yenu, mkitendeana haki kwa dhati;

6. kama mkiacha kuwadhulumu wageni, yatima au wajane au kuwaua watu wasio na hatia katika nchi hii; kama mkiacha kuabudu miungu mingine na kujiangamiza wenyewe,

7. basi mimi nitawaacha daima mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa wazee wenu tangu zamani.

8. “Lakini kumbe, mnayaamini maneno ya uongo bure.

9. Mnaiba, mnaua, mnafanya uzinzi, mnaapa uongo, mnamfukizia mungu Baali ubani na kuabudu miungu mingine ambayo hamjapata kuijua.

10. Kisha, mnakuja na kusimama mbele yangu, katika hekalu hili linalojulikana kwa jina langu na kusema; ‘Tuko salama,’ huku mnaendelea kufanya mambo hayo yanayonichukiza.

11. Je, hekalu hili linalojulikana kwa jina langu limekuwa pango la wanyanganyi? Jueni kuwa mimi nimeyaona yote mnayofanya!

12. Nendeni mahali pangu kule Shilo, mahali nilipopachagua niabudiwe hapo awali, mkaone maangamizi niliyoyafanya huko kwa sababu ya uovu wa watu wangu, Israeli.

13. Nyinyi mmefanya mambo hayo yote, na hata niliposema nanyi tena na tena hamkunisikiliza. Nilipowaiteni hamkuitika.

14. Kwa hiyo, kama nilivyoutendea mji wa Shilo, ndivyo nitakavyolitendea hekalu hili linalojulikana kwa jina langu, hekalu ambalo nyinyi mnalitegemea; naam, mahali hapa ambapo niliwapa nyinyi na wazee wenu.

15. Nitawafukuzeni mbali nami kama nilivyowatupilia mbali ndugu zenu, wazawa wote wa Efraimu.

16. “Nawe, Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, usiwaombee dua wala usinisihi kwa ajili yao, maana sitakusikiliza.

17. Je, wewe huoni mambo wanayofanya katika miji ya Yuda na katika mitaa ya Yerusalemu?

Kusoma sura kamili Yeremia 7