Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 7:27-34 Biblia Habari Njema (BHN)

27. “Basi, wewe Yeremia utawaambia maneno haya yote, lakini wao hawatakusikiliza. Utawaita, lakini hawatakuitikia.

28. Utawaambia; ‘Nyinyi ni taifa ambalo halikutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wala kukubali kuwa na nidhamu. Kwenu uaminifu umekufa; umetoweka kabisa katika maneno yenu.’

29. “Nyoeni nywele zenu enyi wakazi wa Yerusalemu, mzitupe;fanyeni maombolezo juu ya vilele vya milima,maana, mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa nyinyi,mlio kizazi kilichosababisha hasira yangu!

30. “Watu wa Yuda wametenda uovu mbele yangu. Wameweka vinyago vyao vya kuchukiza ndani ya nyumba hii ijulikanayo kwa jina langu, wakaitia unajisi.

31. Wamejenga madhabahu iitwayo ‘Tofethi’ huko kwenye bonde la mwana wa Hinomu, wapate kuwachoma sadaka watoto wao wa kiume na wa kike humo motoni. Mimi sikuwa nimewaamuru kamwe kufanya jambo hilo, wala halikunijia akilini mwangu.

32. Kwa sababu hiyo, siku zaja ambapo hawataliita tena ‘Tofethi,’ au ‘Bonde la Mwana wa Hinomu,’ bali wataliita ‘Bonde la Mauaji.’ Huko ndiko watakakozika watu, kwa sababu hapatakuwa na mahali pengine pa kuzikia.

33. Maiti za watu hao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa porini, na hapatakuwa na mtu atakayewafukuza.

34. Nchi itakuwa jangwa na katika miji ya Yuda na mitaa ya Yerusalemu nitakomesha sauti zote za vicheko na furaha, sauti za bwana arusi na bibi arusi, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.

Kusoma sura kamili Yeremia 7