Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 4:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Hadi lini nitaona bendera ya vitana kuisikia sauti ya tarumbeta?

22. Mwenyezi-Mungu asema:“Watu wangu ni wapumbavu,hawanijui mimi.Wao ni watoto wajinga;hawaelewi kitu chochote.Ni mabingwa sana wa kutenda maovu,wala hawajui kutenda mema.”

23. Niliiangalia nchi, lo! Imekuwa mahame na tupu;nilizitazama mbingu, nazo hazikuwa na mwanga.

24. Niliiangalia milima, lo, ilikuwa inatetemeka,na vilima vyote vilikuwa vinayumbayumba.

25. Nilikodoa macho wala sikuona mtu;hata ndege angani walikuwa wametoweka.

26. Niliona nchi yenye rutuba imekuwa jangwa,na miji yake yote imekuwa magofu matupu,kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu.

27. Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Nchi nzima itakuwa jangwa tupu;lakini sitaiharibu kabisa.

28. Kwa hiyo, nchi itaomboleza,na mbingu zitakuwa nyeusi.Maana, nimetamka na sitabadili nia yangu;nimeamua, wala sitarudi nyuma.

29. Watakaposikika wapandafarasi na wapiga mishale,kila mmoja atatimua mbio.Baadhi yao watakimbilia msituni,wengine watapanda majabali.Kila mji utaachwa tupu;hakuna mtu atakayekaa ndani.

30. Nawe Yerusalemu uliyeachwa tupu,unavalia nini mavazi mekundu?Ya nini kujipamba kwa dhahabu,na kujipaka wanja machoni?Unajirembesha bure!Wapenzi wako wanakudharau sana;wanachotafuta ni kukuua.

31. Nilisikia sauti kama ya mwanamke anayejifungua,yowe kama anayejifungua mtoto wa kwanza.Ilikuwa sauti ya Yerusalemu akitweta,na kuinyosha mikono yake akisema,‘Ole wangu!Wanakuja kuniua!’”

Kusoma sura kamili Yeremia 4