Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 34:11-19 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Lakini baadaye walibadili nia zao, wakawashika tena watumwa hao wa kiume na wa kike ambao walikuwa wamewaacha huru, wakawafanya watumwa.

12. Hapo neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yeremia:

13. “Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Nilifanya agano na wazee wenu nilipowatoa nchini Misri ambako walikuwa watumwa, nikawaambia:

14. ‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu atamwacha huru ndugu yake Myahudi aliyeuzwa akawa mtumwa kwa muda wa miaka sita. Mnapaswa kuwaacha huru, wasiwatumikie tena.’ Lakini wazee wenu hawakunisikiliza wala kunitegea sikio.

15. Hivi karibuni nyinyi mlitubu, mkafanya mambo yaliyo sawa mbele yangu, mkawaacha huru Waisraeli wenzenu na kufanya agano mbele yangu katika nyumba yangu.

16. Lakini baadaye mligeuka, mkalitia unajisi jina langu, wakati mlipowachukua tena watumwa walewale wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaachia kama walivyotaka, mkawalazimisha kuwa watumwa tena.

17. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi hamkunitii kuhusu kuwapatia uhuru ndugu zenu Waisraeli. Basi, nami pia nitawapatieni uhuru; uhuru wa kuuawa kwa upanga vitani, kuuawa kwa maradhi na kwa njaa. Nitawafanya muwe kioja kwa falme zote duniani.

18. Watu waliovunja agano langu na kukataa kufuata masharti ya agano walilofanya mbele yangu, nitawafanya kama yule ndama waliyemkata sehemu mbili na kupita katikati yake.

19. Watu hao ndio hao maofisa wa Yuda, maofisa wa mji wa Yerusalemu, matowashi, makuhani, pamoja na wananchi wote waliopita katikati ya sehemu mbili za yule ndama.

Kusoma sura kamili Yeremia 34