Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 32:35-44 Biblia Habari Njema (BHN)

35. Walimjengea mungu Baali madhabahu katika bonde la Mwana wa Hinomu, ili wamtolee mungu Moleki wavulana wao na binti zao, ingawa sikuwaamuru wala sikufikiria kwamba wangefanya hivyo, wakawafanya watu wa Yuda watende dhambi.”

36. Sasa basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Yeremia, watu hawa wanasema kwamba, kwa vita, njaa na maradhi, mji huu utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni. Lakini nasema:

37. Nitawakusanya watu kutoka nchi zote ambako kwa hasira na ghadhabu na chuki yangu kubwa, niliwatawanya. Nitawarudisha tena mahali hapa, na kuwafanya wakae salama.

38. Nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.

39. Nitawapa moyo mmoja na nia moja, wapate kunicha mimi daima, kwa faida yao wenyewe na kwa faida ya watoto wao watakaofuata.

40. Nitafanya nao agano la milele, kwamba sitaacha kamwe kuwatendea mema; nitaweka mioyoni mwao uchaji wangu ili wasiniache tena.

41. Nitafurahi kuwatendea mema; nitawasimika daima katika nchi hii na kuwatendea kwa uaminifu.

42. “Kama nilivyowaletea maafa watu hawa, ndivyo nitakavyowaletea mema niliyowaahidi.

43. Mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo unasema imekuwa ukiwa bila watu wala wanyama, na kwamba imetolewa kwa Wakaldayo.

44. Watu watanunua mashamba kwa fedha, watazitilia sahihi hati zake za kuyamiliki, watazipiga mhuri, na kuweka mashahidi katika nchi ya Benyamini, kandokando ya Yerusalemu, katika miji ya Yuda, katika miji ya nchi ya milima, katika miji ya Shefela, na katika miji ya jangwa la Negebu. Maana nitawastawisha tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kusoma sura kamili Yeremia 32