Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 31:21-35 Biblia Habari Njema (BHN)

21. “Weka alama katika njia zako,simika vigingi vya kukuongoza,ikumbuke vema ile njia kuu,barabara uliyopita ukienda.Ewe Israeli rudi,rudi nyumbani katika miji yako.

22. Utasitasita mpaka liniewe binti usiye mwaminifu?Maana, mimi nimefanya kitu kipya duniani:Mwanamke amtafuta mwanamume.”

23. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nitakapowafanikisha tena watu wa Israeli, wao watatangaza tena katika nchi ya Yuda na katika miji yake wakisema:‘Mwenyezi-Mungu akubariki ewe makao adili,akubariki ee mlima mtakatifu!’

24. “Ndipo watu wa Yuda na miji yake yote, wakulima na wachungaji wanaopitapita na makundi yao, watakaa huko pamoja.

25. Waliochoka nitawachangamsha, na walegevu nitawapa nguvu.

26. Ndio maana mtu ataweza kusema: ‘Niliamka nikatambua kwamba usingizi wangu ulinifaa sana.’”

27. Mwenyezi-Mungu asema: “Tazama, siku zaja ambapo nitaijaza nchi ya Israeli na nchi ya Yuda watu na wanyama kama mkulima asiavyo mbegu.

28. Na kadiri nilivyokuwa mwangalifu kuwangoa, kuwabomoa, kuwaangusha, kuwaharibu na kuwatesa, ndivyo nitakavyokuwa mwangalifu kuwapanda na kuwajenga.

29. Siku hizo watu hawatasema tena:‘Wazee walikula zabibu chungu,na meno ya watoto yakatiwa ganzi.’

30. La! Kila mmoja atakufa kwa sababu ya dhambi zake mwenyewe; ni yule tu atakayekula zabibu mbivu ndiye meno yake yatatiwa ganzi.”

31. Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda.

32. Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na wazee wao nilipowatoa kwa mkono wangu kutoka Misri; agano hilo walilivunja, ingawa mimi nilikuwa Bwana wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

33. Baada ya siku hizo, nitafanya agano lifuatalo na Waisraeli: Nitaiweka sheria yangu ndani yao, na kuiandika katika mioyo yao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

34. Wala haitawabidi kufundishana na kusema: ‘Mjue Mwenyezi-Mungu’, kwa sababu wote, wadogo kwa wakubwa, watanijua mimi Mungu. Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.”

35. Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi, aliyepanga jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku, na aifanyaye bahari iwe na mawimbi:

Kusoma sura kamili Yeremia 31