Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 29:21-32 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi juu ya Ahabu mwana wa Kolaya, na juu ya Sedekia mwana wa Maaseya, ambao wanawatabirieni uongo kwa jina lake: “Nitawatia mikononi mwa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, naye atawaua mkiona kwa macho yenu wenyewe.

22. Kwa sababu jambo hilo litakalowapata, watu wote waliohamishiwa Babuloni kutoka Yerusalemu watatumia msemo huu wa kulaania: Mwenyezi-Mungu akufanye kama Sedekia na Ahabu, ambao mfalme wa Babuloni aliwachoma motoni.

23. Kisa ni kwamba walitenda mambo ya aibu katika Israeli. Walizini na wake za jirani zao, na kusema maneno ya uongo kwa jina langu, jambo ambalo mimi sikuwaamuru walifanye. Mimi nayajua hayo; nimeyashuhudia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

24. Mwenyezi-Mungu aliniagiza nimwambie hivi Shemaya wa Nehelamu:

25. “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Umepeleka barua kwa jina lako kwa wakazi wote wa Yerusalemu na kwa kuhani Sefania mwana wa Maaseya na kwa makuhani wengine wote. Katika barua hiyo, ulimwambia Sefania hivi:

26. ‘Mwenyezi-Mungu amekufanya wewe Sefania kuwa kuhani badala ya kuhani Yehoyada, uwe mkuu wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Ni wajibu wako kumtia gerezani na kumfunga minyororo mwendawazimu yeyote anayetabiri.

27. Kwa nini basi, hukumkemea Yeremia kutoka Anathothi anayekutabiria?

28. Maana yeye alituma taarifa huko Babuloni kwamba uhamisho wenu utakuwa wa muda mrefu, na kusema mjenge nyumba, mkae; mlime mashamba, mpande mbegu na kula mazao yake!’”

29. Kuhani Sefania aliisoma barua hiyo mbele ya nabii Yeremia.

30. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Yeremia:

31. “Wapelekee watu wote walioko uhamishoni ujumbe huu: Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Shemaya wa Nehelamu: Shemaya amewatabirieni, hali mimi sikumtuma, akawafanya muuamini uongo.

32. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitamwadhibu Shemaya wa Nehelamu pamoja na wazawa wake. Hakuna hata mmoja wa watu wake atakayebaki hai kuona mema nitakayowafanyia watu wangu, kwa sababu amewachochea watu waniasi mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kusoma sura kamili Yeremia 29