Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 27:10-21 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Hao wanawatabirieni uongo na hii itasababisha mhamishwe mbali na nchi yenu. Nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia.

11. Lakini watu wa taifa lolote litakalomtii mfalme wa Babuloni na kumtumikia, nitawaacha wakae nchini mwao, wailime ardhi yao na kuishi humo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

12. Mimi Yeremia nilikuwa nimemwambia Sedekia mfalme wa Yuda, mambo hayohayo. Nilimwambia: “Mtii mfalme wa Babuloni. Mtumikie yeye na watu wake, nawe utaishi.

13. Ya nini wewe na watu wako kufa kwa vita, njaa na maradhi? Maana, hivyo ndivyo alivyosema Mwenyezi-Mungu kuhusu yatakayolipata taifa lolote litakaloacha kumtumikia mfalme wa Babuloni.

14. Usisikilize maneno ya manabii wanaokuambia: ‘Usimtumikie mfalme wa Babuloni’, kwa sababu wanakutabiria uongo.

15. Mwenyezi-Mungu anasema: ‘Mimi sikuwatuma manabii hao, bali wanatabiri uongo kwa jina langu. Kwa hiyo nitawafukuzia mbali, nanyi mtaangamia, pamoja na hao manabii wanaowatabirieni uongo.’”

16. Kisha, niliwaambia makuhani na watu wote: Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Msiwasikilize manabii wenu wanaowatabiria wakisema: ‘Tazama, vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu vitarudishwa hivi karibuni kutoka Babuloni’, kwa maana wanawadanganyeni.

17. Msiwasikilize. Mtumikieni mfalme wa Babuloni, nanyi mtaishi. Ya nini mji huu ufanywe kuwa magofu?

18. Ikiwa wao ni manabii, na kama wana neno la Mwenyezi-Mungu, basi, na wamsihi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili vyombo vilivyobaki katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika nyumba ya mfalme wa Yuda, na katika mji wa Yerusalemu, visichukuliwe na kupelekwa Babuloni.

19. Kwa maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi juu ya nguzo, sinia za shaba, vinara na vyombo vingine vilivyoachwa katika mji huu

20. ambavyo Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, hakuvichukua wakati alipowachukua Yekonia mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda na waheshimiwa wote wa Yuda na Yerusalemu kutoka Yerusalemu na kuwapeleka uhamishoni.

21. “Sikilizeni mambo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, ninasema juu ya vile vyombo vilivyoachwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika nyumba ya mfalme wa Yuda na katika mji wa Yerusalemu.

Kusoma sura kamili Yeremia 27