Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 11:8-15 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Lakini wao hawakunitii, wala hawakunisikiliza. Badala yake, kila mmoja wao alizidi kuwa mkaidi na mwovu. Basi, niliwaadhibu kulingana na masharti ya agano hili nililowaamuru walishike, lakini hao wakakataa kulishika.”

9. Tena Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wanafanya njama za kuniasi.

10. Wameurudia uovu wa wazee wao ambao walikataa kusikiliza maneno yangu; wameiabudu miungu mingine na kuitumikia. Watu wa Israeli na watu wa Yuda wamevunja agano nililofanya na wazee wao.

11. Kwa hiyo, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu ninawaonya kwamba nitawaletea maafa ambayo hawataweza kuepukana nayo. Hata kama wakinililia namna gani, sitawasikiliza.

12. Hapo ndipo watu wa Israeli na Yerusalemu watakapoiendea miungu yao ambayo wanaifukizia ubani. Lakini miungu hiyo haitaweza kuwaokoa wakati huo wa taabu zao.

13. Miungu yako, ewe Yuda imekuwa mingi kama ilivyo miji yako; kama zilivyo nyingi barabara za Yerusalemu, ndivyo zilivyo nyingi madhabahu walizomjengea mungu kinyaa Baali, ili kumfukizia ubani.

14. Basi, wewe Yeremia, usiwaombee watu hawa, usinililie kwa ajili yao, wala usiwaombee dua. Maana, hata wakiniomba wanapotaabika, mimi sitawasikiliza.”

15. Mwenyezi-Mungu asema: “Watu niwapendao wana haki gani kuingia hekaluni mwangu wakati wametenda maovu? Je, wanadhani nadhiri na nyama zilizowekwa wakfu zitawaondolea maafa? Je, hayo yatawafurahisha?

Kusoma sura kamili Yeremia 11