Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 1:7-19 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia,“Usiseme kwamba wewe ni kijana bado.Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao,na yote nitakayokuamuru utayasema.

8. Wewe usiwaogope watu hao,kwa maana niko pamoja nawe kukulinda.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

9. Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia,“Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako.

10. Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme,uwe na mamlaka ya kungoa na kubomoa,mamlaka ya kuharibu na kuangamiza,mamlaka ya kujenga na ya kupanda.”

11. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Yeremia, unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona tawi la mlozi unaochanua.”

12. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Umeona vizuri, maana niko macho kulitekeleza neno langu.”

13. Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili: “Unaona nini?” Nami nikasema, “Ninaona chungu kinatokota kimeinama upande wangu kutoka kaskazini.”

14. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Maangamizi yataanzia kutoka kaskazini na kuwapata wakazi wote wa nchi hii.

15. Maana naziita falme zote za kaskazini na makabila yote. Wafalme wake wote watakuja na kila mmoja wao ataweka kiti chake cha enzi mbele ya malango ya Yerusalemu na kandokando ya kuta zake zote, na kuizunguka miji yote ya Yuda.

16. Nami nitawahukumu Waisraeli kwa ajili ya uovu wao wote wa kuniacha mimi, wakafukizia ubani miungu mingine na kuabudu sanamu walizojitengenezea wenyewe.

17. Sasa basi, wewe Yeremia jiweke tayari. Haya! Nenda ukawaambie mambo yote ninayokuamuru. Usiwaogope, nisije nikakufanya mwoga mbele yao.

18. Leo hii nakufanya kuwa imara kama mji uliozungukwa na ngome, kama mnara wa chuma na kama ukuta wa shaba nyeusi, dhidi ya nchi yote, dhidi ya wafalme wa Yuda, wakuu wake, makuhani wake na watu wake wote.

19. Watapigana nawe, lakini hawatashinda kwa sababu mimi niko pamoja nawe kukuokoa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kusoma sura kamili Yeremia 1