Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 26:12-28 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Nitatembea kati yenu na kuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu.

13. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa nchini Misri ili msiwe watumwa wa Wamisri. Mimi nimevunja nira mliyofungiwa shingoni mwenu na kuwafanya mtembee wima.

14. “Lakini kama hamtanisikiliza wala kufuata amri zangu,

15. kama mkidharau masharti yangu na kuchukia kwa roho maagizo yangu mkaacha kuzitii amri zangu zote na kuvunja agano langu,

16. basi, mimi nitafanya hivi: Nitawapiga kwa kuwaletea hofu kuu ya ghafla, kifua kikuu na homa itakayowapofusha macho na kuwadhoofisha. Mtapanda mbegu zenu bila mafanikio kwani adui zenu ndio watakaokula.

17. Mimi nitawakabili, nanyi mtapigwa na adui zenu; mtatawaliwa na wale wanaowachukia. Mtatishwa na kukimbia hata kama hakuna mtu yeyote anayewafukuza.

18. Na Kama hata baada ya kuadhibiwa hivyo, hamtanisikiliza, basi, nitawaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.

19. Kiburi chenu nitakivunjilia mbali kwa kuzifanya mbingu huko juu kuwa ngumu kama chuma, na nchi yenu bila mvua iwe ngumu kama shaba.

20. Mtatumia nguvu zenu bure maana mashamba yenu hayatatoa mavuno na nchi yenu haitazaa matunda.

21. “Kama mkiendelea kunipinga na kukataa kunisikiliza, nitazidisha tena adhabu yenu mara saba kadiri ya wingi wa dhambi zenu.

22. Nitawapeleka wanyama wakali kati yenu ambao watawanyakulieni watoto wenu na kula mifugo yenu; na kukata idadi yenu hata njia zenu zigeuke kama jangwa.

23. “Kama hata baada ya adhabu hiyo bado hamnigeukii mimi, ila mnazidi kupingana nami,

24. basi, nami nitapingana nanyi na kuwaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.

25. Nitawaleteeni upanga ambao utalipiza kisasi juu ya agano mlilovunja. Nyinyi mtakimbilia katika miji yenu, lakini nitawapelekea maradhi mabaya na kuwatia mikononi mwa adui zenu.

26. Chakula chenu nitakipunguza hata wanawake kumi watumie jiko moja tu kuoka mikate. Watawagawia kwa kipimo. Na hata baada ya kula bado mtakuwa na njaa tu.

27. “Na kama hata baada ya hayo yote bado hamtanisikiliza mkaendelea kunipinga,

28. basi nami nitapingana nanyi kwa hasira kali, na kuwaadhibu mimi mwenyewe mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.

Kusoma sura kamili Walawi 26