Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 25:37-51 Biblia Habari Njema (BHN)

37. Usimkopeshe fedha kwa riba au kumpa chakula ili akulipe faida.

38. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa nchini Misri ili kukupa nchi ya Kanaani, na ili nami niwe Mungu wako.

39. “Kama ndugu yako anayeishi karibu nawe amekuwa maskini, akijiuza kwako, usimfanye akutumikie kama mtumwa.

40. Atakaa nawe kama mtumishi aliyeajiriwa au kama msafiri. Atakutumikia hadi mwaka wa kuadhimisha miaka hamsini.

41. Mwaka huo ni lazima umpe uhuru wake arudi kwa jamaa yake na urithi wa wazee wake; mwachie pamoja na jamaa yake.

42. Kwa kuwa Waisraeli ni watumishi wangu ambao niliwatoa nchini Misri, basi, wasiuzwe kama watumwa.

43. Usimtawale ndugu yako kwa ukatili, ila utamcha Mungu wako.

44. Kuhusu watumwa, wa kike na wa kiume, unaweza kuwanunua kutoka kwa watu wa mataifa mengine ya jirani.

45. Unaweza pia kununua watumwa kutoka kwa wageni wanaokaa pamoja nawe na jamaa zao waliozaliwa nchini mwenu; nao watakuwa mali yako.

46. Hao watumwa unaweza kuwakabidhi kwa watoto wako wawe mali yao milele. Hao unaweza kuwafanya watumwa wako, lakini kuhusu ndugu yako Mwisraeli, usimtawale kwa ukatili.

47. “Kama mgeni au msafiri anayekaa miongoni mwenu amekuwa tajiri na ndugu yako akawa maskini na kujiuza kwa huyo mgeni au huyo msafiri au kwa mmoja wa jamaa zao,

48. anaweza kukombolewa baada ya kujiuza; mmojawapo wa ndugu zake anaweza kumkomboa.

49. Mjomba wake anaweza pia kumkomboa, au binamu yake au ndugu wa karibu katika ukoo wake; anaweza pia kujikomboa yeye mwenyewe kama akiwa tajiri.

50. Yeye akishirikiana na yule aliyemnunua, atahesabu idadi ya miaka tangu alipojiuza mpaka mwaka wa kuadhimisha kukumbuka miaka hamsini. Gharama ya kuachiliwa huru kwake italingana na miaka aliyomtumikia. Muda ambao amekuwa mtumwa wa bwana wake utapimwa kama muda wa mtumishi wa kuajiriwa.

51. Kama idadi ya miaka mpaka mwaka wa ukumbusho wa miaka hamsini ni kubwa zaidi, basi atarudisha kiasi kikubwa cha bei aliyolipiwa.

Kusoma sura kamili Walawi 25