Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 25:21-30 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Haya! Mimi nitaibariki nchi katika mwaka wa sita nayo itawapeni mazao ya kuwatosha kwa miaka mitatu.

22. Mtakapopanda katika mwaka wa nane mtakuwa mnakula mazao ya zamani na mtaendelea kula tu hata mwaka wa tisa mtakapoanza tena kuvuna.

23. “Kamwe ardhi isiuzwe kabisa, kwani hiyo ni mali yangu na nyinyi ni wageni na wasafiri nchini mwangu.

24. Ndiyo maana katika nchi yote mtakuwa na utaratibu wa kuikomboa ardhi.

25. “Kama ndugu yako anakuwa maskini, akauza ardhi yake, basi, ndugu yake wa karibu mwenye jukumu la kuikomboa, ataikomboa.

26. Ikiwa mtu huyo hana ndugu mwenye jukumu la kuikomboa, lakini baadaye akawa tajiri na kupata uwezo wa kuikomboa ardhi yake,

27. basi, atahesabu miaka inayohusika tangu alipoiuza na kulipa gharama zake; na yule mtu aliyeinunua ni lazima amrudishie.

28. Lakini ikiwa hana uwezo wa kuikomboa, basi, itabaki mikononi mwa yule aliyeinunua mpaka mwaka wa sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini. Katika mwaka huo, ni lazima mali hiyo iachiliwe na kurudishiwa yule mtu aliyeiuza.

29. “Kama mtu akiuza nyumba yake ya kuishi iliyo ndani ya mji uliojengewa ukuta, ataweza kuikomboa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu alipoiuza. Kwa mwaka huo mzima atakuwa na haki ya kuikomboa.

30. Kama nyumba iliyo katika mji uliojengewa ukuta haikukombolewa kwa muda wa mwaka mmoja, basi, itakuwa mali ya yule aliyeinunua milele katika vizazi vyao vyote; wala haitarudishwa katika mwaka wa sikukuu ya kukumbuka miaka hamsini.

Kusoma sura kamili Walawi 25