Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 25:17-35 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Msipunjane, bali, mtamcha Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

18. “Kwa hiyo, mtafuata masharti yangu na kutekeleza maagizo yangu, ili mpate kuendelea kuishi kwa usalama katika nchi.

19. Nchi itatoa mazao yake nanyi mtakula na kushiba na kuishi humo kwa usalama.

20. Lakini labda mtafikiri, ‘Tutakula nini katika mwaka wa saba iwapo haturuhusiwi kupanda wala kuvuna mazao yetu?’

21. Haya! Mimi nitaibariki nchi katika mwaka wa sita nayo itawapeni mazao ya kuwatosha kwa miaka mitatu.

22. Mtakapopanda katika mwaka wa nane mtakuwa mnakula mazao ya zamani na mtaendelea kula tu hata mwaka wa tisa mtakapoanza tena kuvuna.

23. “Kamwe ardhi isiuzwe kabisa, kwani hiyo ni mali yangu na nyinyi ni wageni na wasafiri nchini mwangu.

24. Ndiyo maana katika nchi yote mtakuwa na utaratibu wa kuikomboa ardhi.

25. “Kama ndugu yako anakuwa maskini, akauza ardhi yake, basi, ndugu yake wa karibu mwenye jukumu la kuikomboa, ataikomboa.

26. Ikiwa mtu huyo hana ndugu mwenye jukumu la kuikomboa, lakini baadaye akawa tajiri na kupata uwezo wa kuikomboa ardhi yake,

27. basi, atahesabu miaka inayohusika tangu alipoiuza na kulipa gharama zake; na yule mtu aliyeinunua ni lazima amrudishie.

28. Lakini ikiwa hana uwezo wa kuikomboa, basi, itabaki mikononi mwa yule aliyeinunua mpaka mwaka wa sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini. Katika mwaka huo, ni lazima mali hiyo iachiliwe na kurudishiwa yule mtu aliyeiuza.

29. “Kama mtu akiuza nyumba yake ya kuishi iliyo ndani ya mji uliojengewa ukuta, ataweza kuikomboa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu alipoiuza. Kwa mwaka huo mzima atakuwa na haki ya kuikomboa.

30. Kama nyumba iliyo katika mji uliojengewa ukuta haikukombolewa kwa muda wa mwaka mmoja, basi, itakuwa mali ya yule aliyeinunua milele katika vizazi vyao vyote; wala haitarudishwa katika mwaka wa sikukuu ya kukumbuka miaka hamsini.

31. Lakini nyumba za vijiji ambavyo havikuzungushiwa ukuta zitakuwa chini ya sheria ileile ya ardhi; nyumba hizo zinaweza kukombolewa katika mwaka mmoja lakini ni lazima zirudishwe kwa wenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini.

32. Hata hivyo, nyumba zilizomo katika miji wanayomiliki Walawi zinaweza kukombolewa wakati wowote.

33. Ikiwa mmoja wa Walawi haitumii haki yake ya kukomboa, basi, nyumba iliyouzwa ni lazima irudishwe kwa mwenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini, kwani nyumba zilizomo katika miji wanayomiliki Walawi wamepewa kama sehemu yao kutoka kwa watu wa Israeli.

34. Lakini mashamba wanayomiliki Walawi kwa pamoja, yasiuzwe, kwani huo ni urithi wao wa kudumu.”

35. “Kama ndugu yako amekuwa maskini hata asiweze kujitunza mwenyewe akiwa pamoja nawe, ni lazima umtunze aendelee kuishi nawe; mtendee kama mgeni au msafiri aliye kwako.

Kusoma sura kamili Walawi 25