Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 25:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose huko mlimani Sinai,

2. “Waambie Waisraeli hivi: Mtakapofika katika nchi ninayowapeni mimi Mwenyezi-Mungu kila mwaka wa saba nchi itapumzishwa isilimwe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu.

3. Kwa muda wa miaka sita mtailima nchi, mtapanda, mtapogoa mizabibu yenu na kuvuna mazao yenu.

4. Lakini mwaka wa saba utakuwa ni sabato ya mapumziko rasmi; ni sabato ya Mwenyezi-Mungu. Msipande chochote wala kuipogoa mizabibu yenu.

5. Chochote kinachoota peke yake msikivune wala kuchuma zabibu kutoka miti isiyopogolewa. Huo utakuwa mwaka wa kuipumzisha ardhi rasmi.

6. Hata hivyo mwaka huo wa pumziko rasmi kwa nchi utawapa chakula nyinyi wenyewe, watumwa wenu wa kiume na wa kike, watu mliowaajiri na wageni wanaokaa miongoni mwenu.

7. Nchi itailisha mifugo yenu na wanyama wa porini wanaokaa miongoni mwenu.

8. “Mtahesabu miaka saba mara saba na jumla yake ni miaka arubaini na tisa.

9. Kisha, katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ambayo ni siku ya kufanyiwa upatanisho mtamtuma mtu kupiga tarumbeta katika nchi yote.

10. Mwaka wa hamsini mtauheshimu kwa kutangaza uhuru kwa watumwa wote nchini. Mwaka huo utakuwa ni sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini. Kila mmoja wenu atairudia mali yake na jamaa yake.

11. Kwa kuwa mwaka huo, ni wa sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini, msipande mbegu au kuvuna chochote kiotacho chenyewe wala kuchuma zabibu kutoka miti msiyoipogoa.

12. Mwaka huo ni wa sikukuu kwenu; utakuwa mwaka mtakatifu. Hivyo mtakula yale yanayoota yenyewe mashambani.

13. “Katika mwaka huo chochote ambacho kiliuzwa ni lazima kirudishwe kwa mwenyewe.

14. Unaponunua au kuuza ardhi kwa jirani usimpunje.

15. Bei ya ardhi ni lazima ilingane na miaka kabla ya kurudishwa kwa mwenyewe.

16. Kama miaka inayohusika ni mingi utaongeza bei na kama miaka hiyo ni michache utapunguza bei, kwani bei yake itapimwa kulingana na mazao anayokuuzia.

17. Msipunjane, bali, mtamcha Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Kusoma sura kamili Walawi 25