Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 22:14-33 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Kama mtu mwingine akila vyakula vitakatifu bila kujua, basi, atalipa asilimia ishirini ya thamani ya alichokula na kumrudishia kuhani.

15. Kuhani asivitie unajisi vitu ambavyo Waisraeli wamemtolea Mwenyezi-Mungu

16. na hivyo kusababisha watu wawajibike uovu na hatia yao kwa kula vitu vyao vitakatifu. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayeviweka wakfu vitu hivyo.”

17. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

18. “Mwambie Aroni na wanawe makuhani na Waisraeli wote hivi: Kama mtu yeyote miongoni mwenu au mgeni yeyote aishiye katika Israeli akitoa sadaka yake, iwe ni ya kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari ya kumtolea Mwenyezi-Mungu kwa kuteketezwa,

19. ili apate kukubalika, atatoa katika ng'ombe dume au katika kondoo dume asiye na dosari.

20. Ni marufuku kutoa chochote kilicho na dosari kwani hakitakubaliwa kwa faida yenu.

21. Mtu yeyote anapomtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya amani ili kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari kutoka katika kundi lake la mifugo, ili akubaliwe ni lazima awe ni mnyama mkamilifu; mnyama huyo asiwe na dosari yoyote.

22. Usimtolee Mwenyezi-Mungu mnyama yeyote aliye kipofu, kilema, aliyevunjika mahali, anayetokwa na usaha, mwenye upele au ukurutu, wala usiwatoe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu.

23. Fahali au mwanakondoo aliye na kiungo kimoja kirefu au kifupi kuliko kawaida waweza kumtoa sadaka ya hiari; lakini huyo usimtoe kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri.

24. Mnyama ambaye kiungo chake cha kiume kimejeruhiwa, kimepondwa, kimevunjwa au kimekatwa, kamwe usimtolee Mwenyezi-Mungu; usifanye kitu cha namna hiyo nchini mwako.

25. Wala usipokee kutoka kwa wageni wanyama wa namna hiyo na kunitolea mimi Mungu wako kama chakula. Wanyama hao wana dosari kwa vile wamekatwa na hawatakubaliwa kwa faida yenu.”

26. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

27. “Fahali, kondoo dume au beberu akizaliwa atabaki na mama yake kwa siku saba. Lakini tangu siku ya nane anaweza kutolewa kwa Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto.

28. Lakini usimchinje ng'ombe au kondoo siku moja pamoja na ndama wake.

29. Utakaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya shukrani utaitoa kwa namna ambayo itakufanya ukubaliwe.

30. Mnyama huyo ni lazima aliwe siku hiyohiyo; msimbakize mpaka kesho yake asubuhi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

31. “Kwa hiyo mtazishika na kuzitekeleza amri zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

32. Msilikufuru jina langu takatifu, kwani ni lazima niheshimiwe miongoni mwa watu wa Israeli. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu.

33. Mimi ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

Kusoma sura kamili Walawi 22