Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 13:44-59 Biblia Habari Njema (BHN)

44. basi, mtu huyo ana ukoma; yeye ni najisi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ugonjwa wake upo kwenye kichwa chake.

45. “Mwenye ukoma yeyote atavaa nguo zilizochanika, nywele zake hatazichana, na mdomo wake wa juu ataufunika na atapaza sauti akisema, ‘Mimi ni najisi, mimi ni najisi.’

46. Ataendelea kuwa najisi kwa muda wote alio na ugonjwa huo. Yeye ni najisi; naye atakaa peke yake nje ya kambi.”

47. “Kama kuna namna ya upele wa ukoma kwenye vazi, liwe la sufu au kitani,

48. vazi hilo liwe limefumwa au limesokotwa kwa kitani au sufu au ni vazi la ngozi ya aina yoyote ile,

49. iwapo upele huo una rangi ya kijani au nyekundu katika vazi hilo, basi, vazi hilo lina upele. Kwa hiyo ni lazima kumwonesha kuhani.

50. Kuhani atauangalia upele huo na kuliweka vazi hilo kando kwa muda wa siku saba.

51. Siku ya saba atauangalia upele huo. Ikiwa upele huo umeenea katika vazi hilo, liwe ni la kufuma au kusokotwa au la ngozi au la ngozi ya aina yoyote ile, vazi hilo lina upele. Hivyo vazi hilo ni najisi.

52. Kuhani atalichoma moto vazi hilo kwani lina namna ya upele wa ukoma.

53. “Kama kuhani ataona kuwa upele haukuenea katika vazi, basi,

54. ataamuru vazi hilo lifuliwe na kuwekwa kando kwa muda mwingine wa siku saba.

55. Kuhani ataliangalia hilo vazi baada ya kuoshwa. Ikiwa ile alama haijabadilika rangi yake hata ingawa upele haukuenea, basi, vazi hilo ni najisi. Vazi hilo utalichoma moto, iwe alama ya upele ipo nyuma au mbele ya vazi hilo.

56. “Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kufuliwa, basi atararua ile sehemu iliyo na namna ya upele wa ukoma.

57. Kisha, ikiwa hiyo alama inaonekana tena baadaye katika vazi lililofumwa au lililosokotwa au katika kitu chochote cha ngozi, basi upele umeenea. Hapo vazi hilo utalichoma moto.

58. Lakini vazi ambalo upele umetokea baada ya kulifua itabidi lifuliwe mara ya pili na hivyo lipate kuwa safi.”

59. Hiyo ni sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma unaotokea katika vazi la sufu au kitani au lililofumwa au lililosokotwa au la ngozi. Kwa njia hiyo mtaweza kupambanua kati ya vazi lisilo najisi na lile lililo najisi.

Kusoma sura kamili Walawi 13