Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 13:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni,

2. “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au kipaku mwilini mwake, ikadhihirika kwamba ni ukoma, basi, ataletwa kwa kuhani Aroni au mmoja wa wanawe aliye kuhani.

3. Kuhani atapakagua mahali palipo na ugonjwa na ikiwa nywele za mahali hapo zimebadilika kuwa nyeupe na ugonjwa wenyewe ukionekana kuwa uko ndani zaidi ya ngozi ya mwili wake, basi, huo ni ukoma. Kuhani akimaliza kumkagua, hivyo atatangaza kuwa mtu huyo ni najisi.

4. Lakini ikiwa kipele hicho, ingawa cheupe hakikuingia ndani sana ya ngozi na wala nywele za mahali hapo hazikubadilika kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba.

5. Siku ya saba, kuhani atamwangalia tena mtu huyo, na ikiwa, kulingana na uchunguzi wa kuhani, ugonjwa huo haujaenea kwenye ngozi yake, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku nyingine saba.

6. “Kuhani atamkagua tena mtu huyo siku ya saba. Kama kulingana na uchunguzi wake, ile sehemu ya ugonjwa imefifia na ugonjwa haujaenea, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; huo ni upele tu. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi.

7. Lakini upele huo ukiwa umeenea kwenye ngozi, baada ya mtu huyo kujionesha kwa kuhani kwa ajili ya kutakaswa kwake, basi, atakuja tena kwa kuhani.

8. Kuhani atamwangalia tena, na kama ule upele umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ukoma.

9. “Kama mtu ameshikwa na ukoma, ataletwa kwa kuhani.

10. Kuhani atamwangalia na kama kuna uvimbe mweupe ambao umezifanya nywele zake ziwe nyeupe na uvimbe huo umegeuka kuwa kidonda kibichi,

11. huo ni ukoma wa muda mrefu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hakuna haja ya kumweka mtu huyo kwa uchunguzi kwani yu najisi tayari.

12. Kama ukoma umemshika na umeenea mwili mzima, toka utosini hadi nyayoni kama atakavyoona kuhani,

13. hapo kuhani atamwangalia. Kuhani akiona kuwa ukoma umemwenea mwili mzima, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi kwa sababu mwili umegeuka kuwa mweupe na hivyo mtu huyo yu safi.

Kusoma sura kamili Walawi 13