Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 10:11-20 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Mtawafundisha Waisraeli masharti yote ambayo nimewaambia kwa njia ya Mose.”

12. Mose akamwambia Aroni na wanawe waliosalia: Eleazari na Ithamari, “Chukueni ile sehemu ya sadaka ya nafaka iliyosalia kutoka sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto; muile karibu na madhabahu bila kutiwa chachu kwa sababu ni takatifu kabisa.

13. Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu hiyo ni haki yako na wazawa wako kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hivyo ndivyo nilivyoamriwa.

14. Lakini kidari ambacho hufanywa nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu na mguu unaotolewa sadaka kama ishara, mnaweza kula mahali popote pasipo najisi. Utakula wewe, na watoto wako wa kiume na wa kike. Vitu hivyo umepewa kama haki yako na ya wazawa wako kutoka sadaka za amani za watu wa Israeli.

15. Ule mguu uliotolewa na kidari cha sadaka ya kufanyia ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu watavileta pamoja na sadaka za mafuta zitolewazo kwa moto, ili kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu, viwe sadaka ya kutolewa kwa ishara. Hivyo vitakuwa vyako pamoja na wanao; ni haki yenu milele kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru.”

16. Basi, Mose alichunguza kwa makini kuhusu mbuzi mmoja aliyetolewa sadaka ya kuondoa dhambi, kumbe akagundua kuwa alikwisha teketezwa. Hivyo akawakasirikia sana Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliosalia, akawauliza,

17. “Kwa nini hamkumla katika mahali patakatifu kwa vile huyo ni kitu kitakatifu kabisa na mlikuwa mmepewa huyo ili kuondoa hatia ya jumuiya na kuwafanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu?

18. Tena, kwa vile damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu, ni dhahiri iliwapasa kumla ndani ya mahali patakatifu kama nilivyoamuru.”

19. Aroni akamwambia Mose, “Tazama, leo wametolea sadaka yao ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hata hivyo mambo haya yamenipata! Tena kama ningekula ile sadaka ya kuondoa dhambi hivi leo, je, ingekubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu?”

20. Mose aliposikia hayo, akaridhika.

Kusoma sura kamili Walawi 10