Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 9:37-50 Biblia Habari Njema (BHN)

37. Gaali akasema tena, “Tazama! Watu wanashuka katikati ya nchi na kikosi kingine kinatoka upande wa Mwaloni wa Waaguzi.”

38. Kisha Zebuli akamwambia, “Majivuno yako yako wapi sasa? Si ni wewe uliyesema, ‘Abimeleki ni nani? Kwa nini tumtumikie?’ Sasa, hao ndio watu uliowadharau; nenda ukapigane nao.”

39. Gaali akatoka akiwaongoza watu wa Shekemu na kupigana na Abimeleki.

40. Gaali akashindwa na kukimbia, huku anafuatiwa na Abimeleki. Watu wengi walijeruhiwa na kuanguka njiani hadi kwenye lango la mji.

41. Abimeleki akakaa Aruma na Zebuli akamfukuza Gaali na ndugu zake kutoka mji wa Shekemu.

42. Siku iliyofuata, Abimeleki alipata habari kwamba watu wa Shekemu wametoka mjini na kwenda mashambani.

43. Akachukua watu wake akawagawa katika vikosi vinne, ili waende kuvizia mashambani. Alipowaona watu wanatoka mjini, akatoka alikojificha akawaua.

44. Abimeleki na kundi lake wakaenda mbio kwenda kulinda lango la mji. Makundi yake mawili mengine yaliwashambulia wale waliokuwa mashambani na kuwaua.

45. Abimeleki alipigana na wakazi wa mji huo siku nzima. Akauteka mji na kuwaua watu wote waliokuwamo humo. Akauteketeza mji kwa moto na kuutia chumvi.

46. Watu wote waliokuwa katika mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, walikimbilia kwenye ngome ya nyumba ya mungu aliyeitwa El-berithi.

47. Abimeleki akaambiwa kuwa watu wote waliokuwa kwenye mnara wa Shekemu wamejikusanya pamoja.

48. Abimeleki na watu wake wakaenda mlimani Salmoni, akachukua shoka akakata tawi la mti na kuliweka begani mwake. Halafu akawaambia wale watu aliokuwa nao waharakishe kufanya kama alivyofanya.

49. Kila mmoja akakata tawi kama lile la Abimeleki. Wakachukua matawi yao na kuyaegemeza kwenye kuta za ngome, wakayatia moto na kuichoma ngome; watu wote wanaume na wanawake wapatao 1,000 waliokuwa katika mnara wa Shekemu wakafa.

50. Kisha Abimeleki akaenda Thebesi, akauzingira na kuuteka.

Kusoma sura kamili Waamuzi 9