Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 9:33-46 Biblia Habari Njema (BHN)

33. Mara jua litakapotoka wakati wa asubuhi, ushambulie mji. Gaali akitoka pamoja na watu wake kuja kukukabili, uwatendee ifaavyo.”

34. Abimeleki aliondoka na watu waliokuwa pamoja naye kuja Shekemu wakati wa usiku. Aliwagawa watu wake katika vikosi vinne na kuvizia huko karibu na mji.

35. Gaali, mwana wa Ebedi, akatoka nje na kusimama kwenye lango la mji, wakati huo Abimeleki na watu wake walitoka mahali walipokuwa wanavizia.

36. Gaali alipomwona akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka vilele vya mlima.” Zebuli akamwambia, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”

37. Gaali akasema tena, “Tazama! Watu wanashuka katikati ya nchi na kikosi kingine kinatoka upande wa Mwaloni wa Waaguzi.”

38. Kisha Zebuli akamwambia, “Majivuno yako yako wapi sasa? Si ni wewe uliyesema, ‘Abimeleki ni nani? Kwa nini tumtumikie?’ Sasa, hao ndio watu uliowadharau; nenda ukapigane nao.”

39. Gaali akatoka akiwaongoza watu wa Shekemu na kupigana na Abimeleki.

40. Gaali akashindwa na kukimbia, huku anafuatiwa na Abimeleki. Watu wengi walijeruhiwa na kuanguka njiani hadi kwenye lango la mji.

41. Abimeleki akakaa Aruma na Zebuli akamfukuza Gaali na ndugu zake kutoka mji wa Shekemu.

42. Siku iliyofuata, Abimeleki alipata habari kwamba watu wa Shekemu wametoka mjini na kwenda mashambani.

43. Akachukua watu wake akawagawa katika vikosi vinne, ili waende kuvizia mashambani. Alipowaona watu wanatoka mjini, akatoka alikojificha akawaua.

44. Abimeleki na kundi lake wakaenda mbio kwenda kulinda lango la mji. Makundi yake mawili mengine yaliwashambulia wale waliokuwa mashambani na kuwaua.

45. Abimeleki alipigana na wakazi wa mji huo siku nzima. Akauteka mji na kuwaua watu wote waliokuwamo humo. Akauteketeza mji kwa moto na kuutia chumvi.

46. Watu wote waliokuwa katika mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, walikimbilia kwenye ngome ya nyumba ya mungu aliyeitwa El-berithi.

Kusoma sura kamili Waamuzi 9