Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 9:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Abimeleki, mwana wa Gideoni, akawaendea ndugu na wana wote wa kabila za mama yake huko Shekemu, akawaambia,

2. “Semeni papa hapa mbele ya wananchi wote wa Shekemu: Lipi ni jema kwenu, kwamba watoto wote sabini wa kiume wa Yerubaali wawatawale au mtoto mmoja? Kumbukeni kuwa mimi ni damu yenu.”

3. Ndugu za mama yake wakatangaza maneno haya kote Shekemu kwa niaba yake, na watu wote wa Shekemu wakaamua kumfuata maana alikuwa ndugu yao.

4. Wakampa vipande sabini vya fedha vilivyokuwa kwenye nyumba ya Baal-berithi ambavyo alivitumia kuwakodi watu wakorofi na watu ovyoovyo ili wamfuate.

5. Akafuatana nao kwenda Ofra kwa baba yake na huko akawaua ndugu zake wote sabini juu ya jiwe moja. Lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubabeli alinusurika, maana alijificha.

6. Wananchi wote wa Shekemu na Beth-milo wakakusanyika kwenye mwaloni ulio karibu na mnara huko Shekemu, wakamfanya Abimeleki kuwa mfalme wao.

7. Yothamu alipopata habari hizo, alikwenda kusimama juu ya mlima Gerizimu, akasema kwa sauti kubwa, “Nisikilizeni, enyi watu wa Shekemu kama mnataka Mungu awasikilize na nyinyi.

8. Siku moja, miti ilikwenda kujitafutia mfalme. Basi, ikauambia mzeituni, ‘Tawala juu yetu!’

9. Lakini mzeituni ukajibu, ‘Mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha mafuta ambayo huthaminiwa sana na miungu na wanadamu niende kujisumbua kuitawala miti?’

10. Kisha miti ikauambia mtini, ‘Njoo wewe utawale juu yetu.’

11. Lakini mtini ukajibu, ‘Je, mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha matunda mazuri na matamu, niende kujisumbua kuitawala miti?’

12. Halafu miti ikauambia mzabibu, ‘Njoo wewe uwe mtawala juu yetu.’

13. Lakini mzabibu ukajibu, ‘Mnadhani naweza kuacha shughuli yangu ya kuzalisha divai ambayo hufurahisha miungu na wanadamu, niende kujisumbua kuitawala miti?’

14. Mwishowe miti yote ikauendea mti wa miiba na kuuambia, ‘Njoo wewe utawale juu yetu.’

15. Mti wa miiba ukajibu, ‘Kama kweli mnataka kuniteua kuwa mfalme, njoni mkae chini ya kivuli changu. Lakini kama hamtaki kufanya hivyo, basi moto na utoke kwenye miiba yangu na kuiteketeza hata mierezi ya Lebanoni.’”

16. Yothamu akaendelea kusema, “Sasa basi, mnadhani mmefanya Abimeleki mfalme kwa nia njema na uaminifu? Je, mnadhani mmemtendea wema Yerubaali na jamaa yake kama alivyostahili kwa matendo yake?

17. Aghalabu baba yangu alihatarisha maisha yake kwa kuwapigania na kuwakomboa kutoka kwa Wamidiani!

Kusoma sura kamili Waamuzi 9