Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 8:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Watu wa kabila la Efraimu wakamwuliza Gideoni, “Kwa nini umetutendea hivyo? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali.

2. Lakini Gideoni akawajibu, “Mambo niliyofanya mimi si kitu kabisa kama yakilinganishwa na yale mliyoyafanya nyinyi. Walichookota watu wa Efraimu baada ya mavuno ni chema na kizuri kuliko mavuno ya jamaa yangu ya Abiezeri.

3. Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia.

4. Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao.

5. Basi, akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni wenzangu hawa mikate maana wamechoka sana; nami bado ninaendelea kuwafuatia wafalme Zeba na Salmuna wa Midiani.”

6. Lakini viongozi wa Sukothi wakamwuliza, “Kwa nini tuwape mikate nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?”

7. Gideoni akawaambia, “Sawa, lakini Mwenyezi-Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mikononi mwangu, nitaichanachana miili yenu kwa miiba na mbigili za jangwani.”

8. Kutoka huko akawaendea watu wa Penueli, akawaomba namna ileile. Nao watu wa Penueli wakamjibu kama walivyomjibu watu wa Sukothi.

9. Gideoni akawaambia, “Nitakaporudi kwa amani nitaubomoa mnara huu.”

10. Zeba na Salmuna walikuwa huko Karkori pamoja na jeshi lao la watu 15,000 ambao ndio tu waliobaki kutoka jeshi la mashariki, maana wenzao 120,000 waliuawa.

11. Gideoni akafuata njia ya magharibi iliyo mashariki mwa Noba na Yogbeha, akalishambulia jeshi hilo ambalo halikuwa tayari.

12. Wafalme wa Midiani, Zeba na Salmuna walitoroka wakakimbia, lakini Gideoni aliwafuatia, akawakamata na kulitia jeshi lote hofu kubwa.

Kusoma sura kamili Waamuzi 8