Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 4:10-18 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Baraki akayaita makabila ya Naftali na Zebuluni huko Kedeshi; watu 10,000 wakamfuata. Debora akaenda pamoja naye.

11. Wakati huo, Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake ambao ni wazawa wa Hobabu, baba mkwe wa Mose. Alikuwa amepiga hema lake mbali huko kwenye mwaloni wa Zaananimu, karibu na Kedeshi.

12. Sisera alipopata habari kwamba Baraki mwana wa Abinoamu amekwenda mlimani Tabori,

13. alikusanya jeshi lake lote na magari yake mia tisa ya chuma, akaondoka Harosheth-hagoimu, akaenda kwenye mto Kishoni.

14. Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000.

15. Baraki akafanya mashambulizi, naye Mwenyezi-Mungu akamtimua Sisera na jeshi lake lote mbele ya Baraki kwa upanga. Sisera akatoka katika gari lake, akakimbia kwa miguu.

16. Baraki akalifuatia jeshi hilo na magari mpaka Harosheth-hagoimu na kuwaua wanajeshi wote wa Sisera kwa mapanga; hakubaki hata mtu mmoja.

17. Lakini Sisera alikimbia kwa miguu mpaka hemani kwa Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni. Alifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na amani kati ya mfalme Yabini wa Hazori na jamaa ya Heberi.

18. Yaeli akatoka kumlaki Sisera, akamwambia, “Bwana wangu, karibu kwangu, wala usiogope.” Akaingia hemani mwake, akamfunika kwa blanketi.

Kusoma sura kamili Waamuzi 4