Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 4:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya kifo cha Ehudi, Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.

2. Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, ambaye aliishi huko Hazori. Kamanda wa jeshi lake alikuwa Sisera, mwenyeji wa Harosheth-hagoimu.

3. Mfalme Yabini alikuwa na magari ya vita 900 ya chuma. Aliwakandamiza sana Waisraeli kwa miaka ishirini; nao wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie.

4. Wakati huo, kulikuwa na nabii mwanamke aliyeitwa Debora, mke wa Lapidothi, aliyekuwa mwamuzi wa Waisraeli wakati huo.

5. Debora alikuwa na mazoea ya kuketi chini ya mtende uliokuwa kati ya mji wa Rama na mji wa Betheli katika nchi ya milima ya Efraimu. Watu wa Israeli walimjia ili awaamulie mashauri yao.

6. Siku moja alimwita Baraki mwana wa Abinoamu wa Kedeshi katika nchi ya Naftali. Alipokuja alimwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anakuamuru hivi: ‘Nenda ukusanye watu wako mlimani Tabori, uchague watu 10,000 kutoka makabila ya Naftali na Zebuluni.

7. Mimi nitamchochea Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, aje na majeshi na magari yake kupigana nawe kwenye mto Kishoni, na kumtia mikononi mwako.’”

8. Baraki akamwambia Debora, “Kama utakwenda pamoja nami, nitakwenda. Lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.”

9. Debora akamjibu, “Sawa. Nitakwenda pamoja nawe; lakini hutapata heshima yoyote ya ushindi, maana Mwenyezi-Mungu, atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Basi, Debora akafuatana na Baraki kwenda Kedeshi.

10. Baraki akayaita makabila ya Naftali na Zebuluni huko Kedeshi; watu 10,000 wakamfuata. Debora akaenda pamoja naye.

11. Wakati huo, Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake ambao ni wazawa wa Hobabu, baba mkwe wa Mose. Alikuwa amepiga hema lake mbali huko kwenye mwaloni wa Zaananimu, karibu na Kedeshi.

12. Sisera alipopata habari kwamba Baraki mwana wa Abinoamu amekwenda mlimani Tabori,

13. alikusanya jeshi lake lote na magari yake mia tisa ya chuma, akaondoka Harosheth-hagoimu, akaenda kwenye mto Kishoni.

14. Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000.

15. Baraki akafanya mashambulizi, naye Mwenyezi-Mungu akamtimua Sisera na jeshi lake lote mbele ya Baraki kwa upanga. Sisera akatoka katika gari lake, akakimbia kwa miguu.

Kusoma sura kamili Waamuzi 4