Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 20:11-29 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Hivyo wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa moyo mmoja dhidi ya mji wa Gibea.

12. Watu wa makabila ya Israeli wakatuma wajumbe mpaka kila sehemu ya kabila la Benyamini, wakisema, “Je, ni uovu gani huu uliotukia miongoni mwenu?

13. Sasa tupeni hao watu mabaradhuli wa Gibea ili tuwaue na kutokomeza uovu huu kutoka Israeli.” Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwasikiliza ndugu zao, Waisraeli.

14. Basi walikusanyika huko Gibea kutoka katika kila mji wao, ili kupigana na Waisraeli.

15. Watu wa kabila la Benyamini walikusanya kutoka miji yao jeshi la watu 26,000 wenye kutumia silaha, nao wakazi wa mji wa Gibea wakakusanya watu 700 waliochaguliwa.

16. Kati ya watu hao waliochaguliwa kulikuwa na watu 700 waliotumia mkono wa kushoto; kila mmoja aliweza kurusha jiwe kwa kombeo na kulenga unywele bila kukosea.

17. Waisraeli, licha ya wa kabila la Benyamini, walikusanya watu 400,000 wawezao kutumia silaha. Wote walikuwa hodari wa vita.

18. Waisraeli wakaenda Betheli kutaka shauri kwa Mungu, wapate kujua kabila ambalo litakwenda kwanza kupigana na watu wa kabila la Benyamini. Mwenyezi-Mungu alitaja kabila la Yuda liende kwanza.

19. Basi, Waisraeli wakaenda asubuhi, wakapiga kambi yao karibu na mji wa Gibea.

20. Waisraeli wakatoka kupigana na watu wa kabila la Benyamini karibu na Gibea.

21. Watu wa kabila la Benyamini wakatoka nje ya mji wa Gibea wakapigana na Waisraeli, wakawaangusha chini siku hiyo, watu wa Israeli 22,000.

22. Lakini Waisraeli wakajipa moyo, wakajipanga tena kwa vita mahali pale walipojipanga kwa mara ya kwanza.

23. Basi Waisraeli wakaenda juu, wakamlilia Mwenyezi-Mungu mpaka jioni. Kisha wakaomba shauri kwa Mwenyezi-Mungu: “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Nendeni mkapigane nao.”

24. Hivyo siku ya pili Waisraeli wakakaribia kupigana na watu wa kabila la Benyamini.

25. Siku hiyo ya pili watu wa kabila la Benyamini walitoka Gibea na kuwashambulia Waisraeli, wakawaangusha chini Waisraeli 18,000.

26. Watu wote wa jeshi la Waisraeli wakaenda Betheli. Walikaa huko mbele ya Mwenyezi-Mungu wakiomboleza na kufunga mpaka jioni. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.

27. Waisraeli wakamwomba Mwenyezi-Mungu awape shauri. Wakati huo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa huko Betheli.

28. Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Aroni alikuwa na wajibu wa kuhudumu mbele yake. Waisraeli wakamwuliza Mwenyezi-Mungu, “Je, twende tena kupigana na ndugu zetu, watu wa kabila la Benyamini?” Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Nendeni. Kesho nitawatia mikononi mwenu.”

29. Hivyo, Waisraeli wakaweka watu mafichoni kuuzunguka mji wa Gibea.

Kusoma sura kamili Waamuzi 20