Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 18:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku hizo hakukuwa na mfalme katika Israeli. Basi kabila la Dani lilikuwa linatafuta eneo lake lenyewe la kuishi humo, kwani mpaka wakati huo, halikuwa limegawiwa sehemu yake lenyewe miongoni mwa makabila ya Israeli.

2. Hivyo watu wa kabila la Dani walichagua miongoni mwao watu hodari wakawatuma kutoka huko Eshtaoli na Sora wakawaamuru waende kuipeleleza nchi. Basi watu hao wakafika katika nchi ya milima ya Efraimu, nyumbani kwa Mika, wakakaa humo.

3. Walipokuwa nyumbani kwa Mika, waliitambua sauti ya yule kijana Mlawi. Wakamgeukia na kumwuliza, “Nani amekuleta huku? Una shughuli gani hapa?”

4. Yeye akawajibu, “Mika amefanya nami mpango; ameniajiri nami nimekuwa kuhani wake.”

5. Nao wakamwambia, “Tafadhali utuulizie kwa Mwenyezi-Mungu kama tutafanikiwa katika safari yetu.”

6. Yule kuhani akawaambia, “Nendeni kwa amani. Mwenyezi-Mungu anaichunga safari yenu.”

7. Basi, watu hao watano wakaondoka, wakaenda Laishi. Waliwaona watu walioishi huko, na jinsi walivyokaa kwa usalama kama vile watu wa Sidoni. Walikuwa watu watulivu wasio na wasiwasi na hawakupungukiwa mahitaji yoyote nchini. Walikuwa mbali na watu wa Sidoni, na hawakuwa na shughuli yoyote na watu wengine.

8. Basi hao wapelelezi walirudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, nao wakawauliza, “Mmetuletea taarifa gani?”

9. Wao wakasema, “Inukeni twende na kuishambulia nchi hiyo. Tumeiona nchi hiyo, na kweli ni nchi yenye rutuba. Je, mtakaa hapa tu bila kufanya kitu? Msikawie kwenda kuimiliki nchi hiyo.

10. Mtakapofika huko mtakuta watu wasio na wasiwasi wowote. Nchi hiyo ni kubwa, haikupungukiwa chochote na Mungu ameitia mikononi mwetu.”

11. Basi, watu 600 wa kabila la Dani wakiwa na silaha zao za vita wakaondoka kutoka Sora na Eshtaoli

12. wakaenda kupiga kambi yao huko Kiriath-yearimu katika nchi ya Yuda. Ndiyo maana mahali hapo, upande wa magharibi wa Kiriath-yearimu pameitwa Mahane-dani mpaka leo.

13. Kutoka huko wakaelekea nchi ya milima ya Efraimu, wakafika nyumbani kwa Mika.

Kusoma sura kamili Waamuzi 18