Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 11:9-27 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Kama mkinirudisha nyumbani kupigana na Waamoni halafu Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu, mimi nitakuwa kiongozi wenu.”

10. Wale wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu. Hakika tutafanya kama ulivyosema.”

11. Yeftha akafuatana na wazee wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi wao. Yeftha akasema masharti yake huko Mizpa mbele ya Mwenyezi-Mungu

12. Yeftha akapeleka ujumbe kwa mfalme wa Amoni akamwambia, “Una ugomvi gani nasi hata uje kuishambulia nchi yetu?”

13. Mfalme wa Amoni akawajibu hao wajumbe, “Waisraeli walipotoka Misri, walichukua nchi yangu kutoka mto Arnoni hadi mto Yaboki na mto Yordani. Sasa nirudishie nchi hiyo kwa amani.”

14. Yeftha akatuma tena wajumbe kwa mfalme wa Amoni

15. wamwambie kwa niaba yake, “Waisraeli hawakuchukua nchi ya Wamoabu wala nchi ya Waamoni.

16. Lakini Waisraeli walipotoka Misri, walisafiri jangwani hadi bahari ya Shamu mpaka Kadeshi.

17. Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu wakimwomba awaruhusu kupita katika nchi yake, lakini mfalme wa Edomu akakataa. Basi wakamwomba ruhusa mfalme wa Moabu naye pia akakataa. Kwa hiyo Waisraeli wakabaki Kadeshi.

18. Kisha wakasafiri wakipitia jangwani kuzunguka nchi ya Edomu na Moabu mpaka walipofika upande wa mashariki wa Moabu, wakapiga kambi ngambo ya mto Arnoni. Lakini hawakuingia eneo la Moabu. Mto Arnoni ndio uliokuwa mpaka wa Moabu.

19. Hapo Waisraeli walituma wajumbe kwa mfalme Sihoni wa Waamori huko Heshboni wakamwomba awaruhusu kupita katika nchi yake waende katika nchi yao.

20. Lakini Sihoni hakuwakubali Waisraeli wapite katika nchi yake. Basi, Sihoni akakusanya watu wake wote, akapiga kambi huko Yahasa, akawashambulia Waisraeli.

21. Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni pamoja na watu wake mikononi mwa Waisraeli, wakawashinda. Hivyo Waisraeli wakachukua nchi yote ya Waamori ambao walikuwa wanaishi huko.

22. Walilichukua eneo lote la Waamori tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki na tangu jangwani upande wa mashariki hadi mto Yordani magharibi.

23. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akawafukuza Waamori mbele ya Waisraeli. Je, wewe unataka kutunyanganya nchi yetu?

24. Tosheka na kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa. Lakini nchi yoyote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, amewafukuza wakazi wake, akatupa sisi, hiyo ni mali yetu sisi.

25. Je, unadhani wewe una nguvu kuliko Balaki mwana wa Zipora aliyekuwa mfalme wa Moabu? Yeye hakushindana na Waisraeli au kupigana nao.

26. Wakati wote Waisraeli walipoishi mjini Heshboni na vijiji vyake, na mji wa Aroeri na vijiji vyake pamoja na miji yote iliyo ukingoni mwa mto Arnoni kwa muda wa miaka 300, kwa nini hukulikomboa eneo hilo wakati huo?

27. Mimi sijakukosea kitu na ndio maana unafanya kosa unaponishambulia. Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mwamuzi ataamua leo hii kati ya Waisraeli na watu wa Amoni.”

Kusoma sura kamili Waamuzi 11