Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 10:6-18 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu wakatumikia Mabaali, Maashtarothi, na miungu ya Shamu, ya Sidoni, ya Moabu, ya Amoni na ya Wafilisti. Walimwacha Mwenyezi-Mungu na wala hawakumwabudu tena.

7. Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni.

8. Kwa miaka kumi na minane hao waliwatesa na kuwakandamiza Waisraeli walioishi huko Gileadi katika eneo la Waamori mashariki ya mto Yordani.

9. Waamoni nao walivuka mto Yordani kupigana na makabila ya Yuda, Benyamini na Efraimu. Nao Waisraeli wakapata taabu sana.

10. Basi wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, maana tumekuacha wewe Mungu wetu, tukatumikia Mabaali.”

11. Naye Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Je, mimi sikuwakomboa kutoka kwa Wamisri, Waamoni, Waamori, Wafilisti?

12. Wasidoni, Waamaleki na Wamidiani waliwakandamiza nanyi mkanililia, nami nikawakomboa mikononi mwao.

13. Hata hivyo nyinyi mmeniacha, mkatumikia miungu mingine. Kwa hiyo sitawakomboeni tena.

14. Nendeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua. Iacheni hiyo iwakomboe katika taabu zenu!”

15. Lakini Waisraeli wakamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tumetenda dhambi. Tufanye upendavyo, lakini tunakuomba utuokoe leo.”

16. Kisha wakaitupilia mbali miungu ya kigeni, wakamtumikia tena Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia zaidi kuona taabu za Waisraeli.

17. Waamoni wakajikusanya wakapiga kambi yao huko Gileadi. Waisraeli nao wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Mizpa.

18. Waisraeli na viongozi wao wakaulizana, “Ni nani atakayeanza kupigana na Waamoni? Atakayefanya hivyo ndiye atakayekuwa kiongozi wa wakazi wote wa Gileadi.”

Kusoma sura kamili Waamuzi 10