Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 8:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Hivyo, Walawi wakawatuliza watu wote, wakisema, “Tulieni kwani siku ya leo ni takatifu; msihuzunike.”

12. Watu wote wakarudi nyumbani kwao kula na kunywa; wakifurahi na kuwagawia wengine chakula kwa kuwa waliyaelewa yote waliyotangaziwa.

13. Kesho yake, wakuu wa koo pamoja na makuhani na Walawi wakakusanyika kwa Ezra mwandishi, ili kujifunza sheria.

14. Wakagundua kuwa, imeandikwa katika kitabu cha sheria kuwa Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose, kwamba watu wanapaswa kukaa vibandani wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba.

15. Hivyo wakatangaza katika miji yao yote na huko Yerusalemu, wakisema, “Nendeni milimani, mkalete matawi ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti mingineyo ili kujengea vibanda, kama ilivyoandikwa.”

16. Basi, watu wakaenda kuleta matawi, wakajijengea vibanda kila mtu kwenye dari na kwenye baraza ya nyumba yake, kwenye baraza za nyumba ya Mungu, kwenye uwanja wa Lango la Maji na uwanja wa Lango la Efraimu.

17. Watu wote waliorudi kutoka uhamishoni wakatengeneza vibanda wakaishi humo. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza watu kuishi katika vibanda tangu wakati Yeshua, mwana wa Nuni alipokuwa akiishi. Watu walifurahi sana.

18. Kila siku, tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra aliwasomea watu kitabu cha sheria ya Mungu. Waliadhimisha sikukuu hiyo kwa muda wa siku saba, na siku ya nane wakafanya mkutano mkubwa wa kufunga sikukuu, kama ilivyoagizwa.

Kusoma sura kamili Nehemia 8