Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 5:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya muda kulitokea malalamiko miongoni mwa watu, wanaume kwa wanawake, wakiwalalamikia ndugu zao Wayahudi.

2. Kulitokea waliosema, “Tafadhali tupatie nafaka tule ili tuweze kuishi kwa kuwa sisi, wana wetu na binti zetu tu wengi.”

3. Na wengine wakalalamika, “Tumeweka rehani mashamba yetu, mizabibu yetu hata na nyumba zetu ili kupata nafaka kwa sababu ya njaa.”

4. Tena kukawa na hata wale, waliolalamika, wakisema, “Ili kulipa kodi ya mfalme juu ya mashamba na mizabibu yetu, ilitubidi tukope fedha.

5. Lakini sisi ni sawa na Wayahudi wengine; watoto wetu ni sawa na watoto wao. Hata hivyo, tunawalazimisha watoto wetu kuwa watumwa. Baadhi ya binti zetu tayari ni watumwa. Hatuna uwezo wa kuzuia jambo hili kwani mashamba yetu na mizabibu yetu yameporwa na watu wengine.”

6. Niliposikia malalamiko yao, nilikasirika sana.

7. Nikaamua kuchukua hatua. Nikawashutumu wakuu na maofisa, nikawaambia, “Mnawatoza riba ndugu zenu.”

8. Nikasema, “Kulingana na uwezo tulio nao, tumekuwa tukiwanunua tena ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wa mataifa mengine. Lakini sasa hata mnawauza ndugu zenu, nasi tunalazimika kuwanunua!” Basi walinyamaza kimya, bila kuwa na la kujibu.

9. Kisha nikawaambia, “Mnalolifanya ni baya. Je, haiwapasi kumcha Mungu wetu ili kuzuia mataifa mengine yaliyo adui zetu yasitusute?

10. Zaidi ya hayo, mimi mwenyewe, ndugu zangu na watumishi wangu tumewaazima ndugu zetu fedha na nafaka. Na hatutadai riba yoyote.

11. Leo hii na muwarudishie mashamba yao, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na nyumba zao, hata na riba ya fedha, nafaka, divai, na mafuta ambayo nilikuwa ninawatoza.”

12. Wao wakaitikia na kusema, “Tutawarudishia na hatutawadai chochote. Tutafanya kama ulivyosema.” Nikawaita makuhani mbele, na viongozi wote wakaapa mbele ya makuhani kufanya kama walivyoahidi.

13. Nilikunguta kibindo changu na kusema, “Kila mmoja asiyetimiza ahadi hii Mungu na amkungute, amtoe katika nyumba yake na katika kazi yake. Basi, akungutike na kubaki mikono mitupu.” Mkutano mzima ukaitikia, na kusema, “Amina” wakamsifu Mwenyezi-Mungu. Watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.

14. Tangu wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wa nchi ya Yuda kwa miaka kumi na miwili yaani tangu mwaka wa ishirini mpaka mwaka wa thelathini na mbili wa kutawala kwa mfalme Artashasta, sikula chakula kinachostahili kuliwa na mtawala, wala ndugu zangu hawakufanya hivyo.

15. Watawala walionitangulia walikuwa mzigo mzito kwa watu wakiwadai chakula na divai, mbali na kuwadai kuwalipa sarafu za uzito wa shekeli arubaini za fedha. Hata watumishi wao waliwadhulumu watu. Bali, mimi sikufanya hivyo, kwani nilimcha Mungu.

Kusoma sura kamili Nehemia 5