Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 13:10-19 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Tena nikagundua kuwa Walawi hawakupewa haki zao; na matokeo yake ni kwamba Walawi na waimbaji waliokuwa wakifanya kazi hapo awali, sasa walikwisha rudia mashamba yao.

11. Nikawakemea viongozi, nikasema, “Kwa nini nyumba ya Mungu imeachwa?” Niliwakusanya pamoja na kuwarudisha kazini.

12. Kisha, watu wote wa Israeli, wakaanza tena kuleta zaka zao za nafaka, divai na mafuta kwenye ghala.

13. Nikawateua watu wafuatao kuwa watunzaji wa ghala: Kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki na Pedaia Mlawi. Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania akawa msaidizi wao. Walikuwa waaminifu na kazi yao ilikuwa kuwagawia ndugu zao mahitaji yao.

14. Ee, Mungu wangu, nikumbuke kwa ajili ya haya yote na usiyasahau matendo yangu mema niliyofanya kwa ajili ya nyumba yako na kwa ajili ya huduma yako.

15. Wakati huohuo, nikawaona watu wa Yuda wakisindika na kukamua zabibu siku za Sabato. Tena wengine walikuwa wakiwabebesha punda wao nafaka, divai, zabibu, tini na vitu vingine wakivipeleka mjini Yerusalemu. Nikawaonya kuwa hawana ruhusa kuuza vitu siku hiyo.

16. Watu wengine toka mji wa Tiro walileta samaki na bidhaa nyingine mjini Yerusalemu na kuwauzia watu wetu siku ya Sabato.

17. Nikawakemea viongozi wa watu wa Yuda, nikisema, “Uovu gani huu mnaofanya, kuikufuru Sabato?

18. Je, babu zetu hawakufanya uovu wa namna hii hii na kumfanya Mungu wetu kutuletea maafa pamoja na mji huu? Na bado mnaleta ghadhabu yake juu ya watu wa Israeli kwa kuikufuru Sabato.”

19. Hivyo, niliamuru kuwa malango ya mji wa Yerusalemu yafungwe mara Sabato inapoanza jioni, wakati giza linapoanza kuingia, na yasifunguliwe mpaka Sabato imekwisha. Niliweka baadhi ya watumishi wangu kwenye malango na kuwaagiza kuwa kitu chochote kisiletwe mjini siku ya Sabato.

Kusoma sura kamili Nehemia 13